Siku chache
baada ya Padri Anselm Mwang’amba wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Machui,
Zanzibar kumwagiwa tindikali na watu wasiofahamika, hofu nyingine imeibuka
visiwani humo, anaripoti Mwajuma Juma, Zanzibar.
Hofu hiyo inatokana na mlipuko wa bomu
la kienyeji ambao umetokea saa 8:45 usiku wa kuamkia jana katika eneo la
Darajani, Wilaya ya Mjini Unguja.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, alisema
bomu hilo ambalo limetengenezwa kienyeji, lililipuka jirani na duka la Sahara
Store.
“Bomu hili lilirushwa na watu
wasiofahamika waliokuwa katika gari aina ya Pick Up ambayo namba zake
hazikuweza kupatikana kirahisi, yenye rangi ya silver (fedha)...watu hao
walirusha kitu mfano wa soseji na kuangukia kreti za chupa za soda,” alisema.
Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa mlinzi
mmoja aliyekuwepo eneo hilo, Bw. Amour Kassim Amour, alisema kitu hicho baaada
ya kurushwa, kilianza kutoa moshi mwingi, mshindo mkubwa na kuchimba eneo
kilipoangukia bila kuleta madhara.
“Hakuna mtu aliyekufa wala kuumia,
tunaomba wananchi wawe watulivu, waendelee na shughuli zao kama kawaida, Jeshi
la Polisi na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama tumeinarisha ulinzi katika
maeneo yote,” alisema.
Aliongeza kuwa, hadi sasa hakuna mtu
aliyekamatwa kuhusishwa na tukio hilo, upelelezi unaendelea.Kamanda Mkadam aliwataka wananchi watoe ushirikiano kwa jeshi hilo
na kutoa taarifa zitakazosaidia kuwakamata wahusika ambao lengo lao ni kuleta
hofu na taharuki.
No comments:
Post a Comment