Na Hussein Ally
BAADA ya uongozi kufanya mabadiliko ya
sekretarieti ya klabu hiyo, Baraza la Wazee limeibuka na kupinga mabadiliko
hayo.Yanga
imemuengua Katibu, Lawrence Mwalusako na kumwajiri raia wa Kenya, Patrick
Naggi, lakini Baraza la Wazee wamesema hawatambui mabadiliko hayo.
Patrick
aliibuka katika makao makuu ya Yanga jana na kuwafahamisha kuwa amekuja kufanya
kazi ya Katibu Mkuu wa klabu hiyo, baada ya kuomba nafasi hiyo kupitia kwa
kiongozi ambaye hakutaka kumtaja.Baraza la wazee
lilishtuka kusikia ujio wa Katibu huyo na kushangaa mwenendo mzima uliofanyika,
kwani katika katiba ya Yanga hakuna kitu kinachofanyika bila ya baraza hilo kutambulishwa.
Wazee hao baada ya kuona hali hiyo jana
waliamua kutoa tamko kupitia kwa Katibu wa Baraza la Wazee, Yahaya Akilimali
ambaye alisema wao kama wazee hawamtambui
katibu huyo na hawamtaki.Akilimali alisema, shughuli zote za
uongozi ndani ya Klabu ya Yanga kwa mujibu wa katiba zinafanywa na mwanachama
wa Yanga kwa hiyo katibu huyo hajulikani ametokea tawi gani.
"Kwa niaba ya Mwenyekiti wa Baraza
la Wazee, natoa tamko rasmi sisi wazee wa Yanga hatumtaki katibu huyo mpya na
tunataka mara moja arudi kwao," alisema.Alisema kuna mambo makuu matatu, ambayo
wao hawamtaki katibu huyo kwanza wazee wa klabu hiyo hawajafahamishwa, pili
Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo haina taarifa naye, tatu makatibu na wenyeviti
wa Mkoa wa Dar es Salaam
hawajui lolote.
Hata hivyo katibu huyo mpya alipoulizwa
na wazee nani amemleta katika klabu hiyo, alikataa kusema na kumuona huenda
akawa tapeli anataka kuitapeli Yanga.Wazee hao walisema, Yanga si jalala la
kila mtu anayetaka kuongoza anakubaliwa kwa hiyo wamewataka viongozi wenye
lengo baya na Yanga kuacha mara moja tabia hiyo.
Walisema, kitu chochote kinachofanyika
ndani ya Yanga huwa na taratibu, Mwenyekiti huwaita wazee na kuwashauri baadaye
ndiyo linatolewa tamko kama ilivyofanyika
katika malumbano juu ya TV Azam.Yanga mpaka sasa bado haijampata Katibu Mkuu, kwa sasa Mwalusako ndiye
anayekaimu nafasi hiyo baada ya Mwesigwa Selestine kuenguliwa mwaka jana.
No comments:
Post a Comment