05 September 2013

SIMBA KUIKABILI KMKM KESHO



Na Hamisi Miraji
SIMBA kesho inatarajia kujitupa uwanjani dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu ya Grand Malt Zanzibar KMKM, katika mchezo wa kirafiki utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.Mchezo huo utakuwa wa pili kwa timu ya Simba kucheza na timu ya Zanzibar, ambapo wa kwanza walicheza na Mafunzo na kuibuka na ushindi wa mabao 4-3.

Katika mchezo huo mashabiki wa Simba watapata fursa ya kuwatathmini tena wachezaji wao wa kimataifa kutoka Vital O ya Burundi, Hamisi Tambwe na Gilbert Kaze ambapo beki Kaze akionekana kushushiwa mzigo wa lawama katika mechi ya awali.Mchezo huo utakuwa kwa ajili ya maandalizi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo Simba inatarajia kumenyana na Mtibwa Sugar Septemba 14, katika Uwanja wa Taifa.       KMKM wanatarajia kuwatumia wachezaji wake mahiri, Abdi Kassim 'Babi' na Abdalah Shiboli ambao walipata kuwika katika Ligi Kuu Tanzania Bara na timu za Azam na Simba.Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema mchezo huo utakuwa kipimo kizuri kwa timu hiyo, kwani wanakutana na mabingwa wa Zanzibar. "Ni mchezo mzuri kwetu kwani KMKM ni moja ya timu ngumu visiwani Zanzibar kwa hiyo, kocha ataweza kuangalia upungufu wa kikosi chake katika kwenda kwenye mchezo wetu wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar," alisema. 
Alisema Kocha Mkuu wa Simba, Abdalah 'King' Kibadeni bado anajaribu kuangalia vijana wake kwa kuwapa nafasi, hivyo mashabiki wasiwe na wasiwasi kutokana na mechi yao dhidi ya Mafunzo kuruhusu mabao kirahisi.Kiingilio katika mchezo wa kesho kitakuwa sh. 5,000 viti vya kijani, sh. 8,000 viti vya Orange, sh. 15,000 VIP B na sh. 20,000 VIP A.

No comments:

Post a Comment