26 September 2013

VODACOM YAIPIGA 'JEKI' WIZARA YA MICHEZO.Ibrahim Mussa na Theophan Ng'itu
  Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania, jana imekabidhi vifaa vya michezo kwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamduni na Michezo vyenye thamani ya sh.milioni 11,000,000 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa kampuni hiyo, Kelvin Twissa alisema Vodacom ina furaha kushiriki katika mpango unaolenga kutambua na kuendeleza vipaji vya michezo kwa ngazi ya shule nchini.
"Leo (jana) tunahitimisha ahadi tuliyoitoa kwako, kwamba tutakuunga mkono katika kufanikisha jambo hili pia Vodacom, tunatambua juhudi kubwa zinazofanywa na serikali kupitia wizara yako, hivyo nasi tunajisikia furaha kuwa sehemu ya mikakati ya serikali," alisema Twissa.
Aliongeza kuwa Vodacom, inatambua kuwa michezo ni sehemu ya kuzalisha ajira na kwa sababu hiyo hawaoni ugumu wa kuwekeza kwenye michezo, ili kutengeneza fursa za ajira kwa vijana wa kitanzania.
Vodacom ilikabidhi jezi seti 12, mipira 40 na kombe moja kwa Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Fenella Mukangara pia watatoa posho kwa ajili ya waamuzi na wasimamizi watakaoendesha mashindano hayo.
Naye Waziri Mukangara aliishukuru kampuni hiyo kwa kujitolea kushiriki katika kudhamini michezo mbalimbali nchini ikiwemo Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
" Vifaa hivi ambavyo tumevipokea leo(jana) , tutavitumia katika mashindano ya soka yatakayoshirikisha timu 12 kutoka shule za sekondari za Manispaa zote tatu za Mkoa wa Dar es Salaam, Temeke, Ilala na Kinondoni," alisema.
Aliongeza kuwa wamechukua Mkoa wa Dar es Salaam kama mahali pa kuanzia, lakini wizara ingependa mpango huo uendelee katika mikoa yote Tanzania Bara.

No comments:

Post a Comment