Na Florah Temba, Moshi
KIWANDA cha sukari cha TPC kilichopo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro
kinatarajia kuongeza uzalishaji wa sukari kutoka tani 92,000 zilizozalishwa
kipindi cha mwaka 2012/2013, hadi kufikia tani 100,000 kwa kipindi cha mwaka
huu 2013/2014.
Hayo
yalibainishwa na Ofisa mtendaji mkuu na utawala wa kiwanda hicho, Jafary Ally
wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake kuhusiana na hali ya uzalishaji
katika kiwanda hicho.
Jafary
alisema uzalishaji wa sukari katika kiwanda hicho umekuwa ukiongezeka mwaka
hadi mwaka na hivyo katika kipindi cha mwaka huu wanauhakika wa kuongeza
uzalishaji kutoka tani 92,000 hadi kufikia tani 100,000.Alisema
kiwanda hicho kwa siku huzalisha sukari tani 500 na kwamba bado wataendelea
kuongeza nguvu za uzalishaji ili kufanikisha malengo ya Serikali ya kuinua
uchumi kupitia viwanda.
"Wakati
kiwanda hiki kimeanza kilikuwa kinazalisha sukari tani 36,000, uzalishaji huu
umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka na kufikia tani 92,000 na mwaka huu
tunatarajia kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 100,000, uzalishaji ambao
haujawahi kutokea," alisema Jafary.
Alisema
ongezeko la uzalishaji huo wa sukari,litatokana na uzalishaji mzuri wa miwa katika
kipindi cha mwaka huu na kwamba hali hiyo itawawezesha kuvunja rekodi ya
uzalishaji.Alisema
katika kipindi cha mwaka huu waliweza kufuata kanuni za kilimo bora cha miwa
ambacho kimeonesha mafanikio makubwa katika uzalishaji wa miwa.
Alisema
ongezeko la uzalishaji huo linaweza kuwapa fursa ya kushika nafasi ya kwanza
kwa uzalishaji Afrika, kutoka nafasi ya tatu ambayo walishika mwaka jana."Mbinu
za uzalishaji huu mzuri wa miwa ni kufuata kanuni za kilimo bora cha miwa na
hii inaweza kutufanya tushike nafasi ya kwanza Afrika kwa uzalishaji kwani
hatujaongeza ukubwa wa ardhi na tulichofanya ni kuzingatia kanuni,"
alisema.
No comments:
Post a Comment