09 September 2013

MUELEKEO WA TANZANIA KATIKA MIAKA 50 IJAYO


MWANDISHI Mwajuma Juma

UCHUMI wa nchi unakuja kwa wananchi wenye kujituma zaidi katika kufanyakazi za kuleta maendeleo kwa Taifa kwa kutumia rasilimali watu hususan vijana ili kuweza kupata nguvukazi.Lakini uchumi huo unaweza kuporomoka iwapo vijana wenyewe hawatoweza kupewa njia mbadala za kuweza kujiendeleza kimaisha.Tanzania inakoelekea inaweza kukumbwa na matatizo ya kisiasa na kiuchumi katika Serikali zake
.Hivyo jitihada za lazima ziweze kuchukuliwa na Serikali hizo mbili ambazo ni Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) pamoja na kuwa makini sana katika masuala mazima ya kisiasa na kiuchumi.“Kama tunavyojua uchumi wa nchi unakuja kwa wananchi wenye kujituma zaidi katika kufanyakazi za kuleta maendeleo kwa Taifa kwa kutumia rasilimali watu hususan vijana ili kuweza kupata nguvu kazi,” alisema Mkurugenzi Mipango, Sera wa Chama cha Wakulima Tanzania (AFP), Bw. Rashid Mchenga.
Bw.Mchenga anaendelea kusema kuwa lakini leo vijana kama hawaendelezwi kufanya kazi badala yake kutakuwa wanawafungulia maskani na vijiwe basi hakuna hatua yoyote itakayopatikana kimaendeleo.Anasema kuwa inatakiwa watu wafahamu kwamba kama kutakuwa na vijana wengi bila ya kuwa na kazi ni sawa na kuwa na bomu ambalo linasubiri wakati wowote kulipuka.Kwa hivyo basi anaeleza kuwa iko haja ya kuwaandaa vijana kuwa na kazi na kuwapatia ajira rasmi ili wasiyumbe kiuchumi na kimapato yao kwa mwezi na kwa siku.
Hata hivyo anaendelea kusema kwamba iko haja ya kutumia sera ya viwanda ili kuwawezesha vijana kiajira na kufikia malengo yao ya kiuchumi.“Tunapokuwa na ajira za viwanda Taifa litaweza kuajiri kwa kutumia nguvukazi za viwanda vinatoa ajira hususan kwa nguvukazi na kuondoa tatizo la ajira kwa vijana na Taifa kwa ujumla na hapo tutakua tumeepukana na tatizo la ajira,” anasema Bw. Mchenga.
Akizungumza kwa upande wa kisiasa anasema kuwa isipozingatiwa taifa litapata matatizo ya kisiasa lakini hata hivyo wanaweza kuondokana na matatizo hayo pale watakapoweza kuwa na siasa safi ambayo ndiyo inayoleta maendeleo kwa wote na kudumisha amani na utullivu nchini.“Siasa safi ni zile zinazofuata katiba sheria na haki za binaadamu kwa mujibu wa sheria,” anasema.
Anafahamisha kuwa hayo yatakuja zaidi watakapoondoa ubabe wa kisiasa kuondoa siasa za kikabila na za kidini na za kimajimbo na za chuki ili kuondoa siasa za matusi na kujenga tamaduni mkubwa wa kuheshimiana na mdogo kumuheshimu mkubwa.Anasema kuwa hatua hiyo itaweza kufikia malengo mazuri ya kisiasa na kiuchumi na kuweza kulitoa Taifa katika matatizo.
Bw. Mchenga anasema kuwa nchi nyingi duniani zilizokua hazikuwa makini ziliweza kupatwa na matatizo ya kiuchumi na kisiasa na kuyaweka mataifa yao katika matatizo makubwa kwa mfano Sepras imepata matatizo ya kiuchumi kutokana na mabenki yake kukopesha wananchi pesa na badala yake kutoweza kuzirudisha.
Nchi nyingine ni Ugiriki, Ureno, nazo zilipata matatizo ya kiuchumi lakini zote hizi ziliweza kuja kuokolewa na Jumuiya za Muungano wa nchi za Ulaya na ilionekana faida ya Muungano wa Jumuiya ya Ulaya.Hata hivyo anasema kuwa kuna nchi kama Libya, Syria, Iraq, Misri nazo zilipatwa na matatizo ya kisiasa yaliyotokana na siasa chafu za ubaguzi, siasa za umimi, umajimbo, udini.
Anaendelea kusema kuwa tatizo kubwa la kupatikana matatizo ya kisiasa ya nchi zinapoingia katika siasa hizo basi nchi hizo hudhoofika kisiasa na kiuchumi.“Na kwa Tanzania inafaa tukumbuke tulikotoka na tunakokwenda kwa mifumo mizima ya kisiasa na kiuchumi na kama kule Zanzibar maandamano ya kisiasa ya Januari 26 na 27, 2001 maandamano yaliyopoteza watu wengi,” alisema.
Haya yote yanatokana na ubabe wa kisiasa lakini tukiendelea mbele hadi mwisho tunashuhudia ubabe wa kisiasa na siasa chafu za kimajimbo zinaendelea na zina lidhoofisha taifa kila siku zinavyoendelea.Alitaja mifano katika mikoa mbalimbali ya hapa nchini huko Arusha, Iringa, Mtwara, Mbeya na Dar es Salaam kote kumeshuhudiwa mikasa na vituko vya uvunjifu wa amani kama vile kuvunja miundombinu na uharibifu wa mali za watu waliokuwa hawana hatia, mali za Serikali (Umma) na kufikia kuwahujumu waandishi wa habari
Pia sambamba na vurugu za kidini zilizotokeaa Zanzibar na Dar es Salaam zilileta taharuki kwa watu na kufikia kuporomosha uchumi kupitia utalii na kuharibu mfumo mzima wa utalii kwa wote kusita kwa wageni na kuharibu mipango mizima ya Taifa.Hivyo alisema iko haja ya serikali sote mbili kudumisha ulinzi kwa kupitia Jeshi la Polisi (Usalama wa Raia na mali zake)ili kupatiwa elimu zaidi inayoendana na wakati sambamba na kupatiwa vifaa vya kisasa vinavyoendana na wakati ili kuweza wananchi kujua utaifa wao sera ya nchi yao ya amani na utulivu
Aidha anasema kuwa hatua hiyo itaweza kuwafanya wananchi kuelezewa madhara ya kuleta uharibifu wa miundombinu na mali za Serikali na mali za watu binafsi.Anasema kuwa faida ya kudumisha (amani na utulivu) wa nchi na ukizingatia kwa sasa tuna sera ya utalii kwa wote inahitaji ushirikiano wa hali ya juu.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo alimalizia kwa kusema kuwa kwa sasa kufanikiwa kwa Watanzania ni kuwa na raia wema ambao watafuata sheria, katiba na haki za binadamu kwa mujibu wa sheriaKwa mtazamo huo ndiyo itakuwa wamefuta utawala wa sheria na ndio utawala bora na hata kuweza kuepuka kuwepo kwa matukio mbalimbali yanayotokana na ukiukwaji wa utawala bora.

No comments:

Post a Comment