TUME ya Mabadiliko ya Katiba imeundwa
kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83 ambayo ina kazi ya
kukusanya maoni ili kufanikisha kwa Katiba Mpya hapa chini.Tume hiyo yenye
wajumbe 32 ikiongozwa na Mwenyekiti na Jaji Joseph Warioba imekuwa ikifanya
jitihada za kuhakikisha kuwa wananchi wanatoa maoni yao pamoja na makundi maalumu ili yaingizwe
kwenye Katiba mpya hususani baada ya kuchambua rasimu ya Katiba Mpya na kuona
mambo yaliyosahaulika yanayogusa makundi hayo
.Makundi
mbalimbali yalipata fursa ya kuchambua rasimu ya Katiba Mpya na kutoa
mapendekezo yao kuhusiana na mambo wanayotaka
yaongezwe, yaondolewe na mengine kubaki kama
yalivyo, hii imefanyika ili kutoa haki pande zote.Kundi la
walemavu na wanaoishi na virusi vya Ukimwi ni miongoni mwa makundi yaliyopata
nafasi ya kutoa maoni yao ya kuchangia rasimu ya
Katiba Mpya ambapo makundi hayo nayo yalipata fursa ya kuchangia maoni yao kama makundi maalumu.
Mwenyekiti wa
Shirika la Kilimo la Walemavu Songea (SHIKIWASO) ambaye pia ni mlemavu wa
viungo, Bw. Ally Kiponda anasema kuwa awali katika mabaraza ya Katiba makundi
ya walemavu na wanaoishi na Virusi vya Ukimwi hayakupata fursa ya kuingia
kwenye makundi ya kuchangia rasimu ya Katiba Mpya ambayo yalikuwa katika
makundi ya wanawake, vijana na kundi la jiografia ambalo lilijumuisha makundi
yote.
Anasema kuwa
kwa ufadhili wa Shirika la Foundation for Civil Society (FCS) wao waliamua
kuendesha Baraza la Katiba kwa Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (WAVVU) na
walemavu ili kutoa fursa kwa makundi hayo nayo kutoa maoni yao ili yaingizwe
kwenye Katiba Mpya hatua ambayo itaonesha makundi yote yamefikiwa.
Akichangia
kwenye mkutano wa Baraza la Katiba uliofanyika kwenye Ukumbi wa Maktaba mjini
Songea mmoja wa walemavu, Bw. Samwel Mapunda anapendekeza suala la walemavu
kupata elimu bure kuanzia elimu ya awali hadi chuo kikuu.
Pia vifaa
maalumu kama fimbo nyeupe liingizwe kwenye
Katiba Mpya huku pia akisema katiba itamke haki ya kupata ajira kwa walemavu na
kuwepo uwakilishi kwa wenye ulemavu kuanzia ngazi ya kitongoji hadi Taifa.
"Katiba
pia itamke kuwa walemavu wapate huduma za afya bure na kutengewa eneo la kupata
huduma hizo bure bila bughudha na pia wapatiwe vifaa vya kujimudu ili waweze
kupata huduma nyingine muhimu kwa maisha yao
na kuchangia pato la Taifa," anasema.
Akichangia
kwenye mkutano huo mlemavu mwingine Bw. Christopher Mwamalili ametaka kuwepo na
usawa wa masuala mbalimbali kwa walemavu na kwamba suala hilo liwepo kikatiba si kwa kuzungumzwa tu
mdomoni.
Anasema kuwa
kunatakiwa kuwepo kwa usawa wa viti vya wanawake vya uwakilishi bungeni lakini
kundi la walemavu limekuwa na uwakilishi kwa kiasi kidogo sana.
Mchangiaji
mwingine Bw.Kasim Mngwali ametaka a s a s i za kuwahudumia walemavu zisiwatumie
walemavu kama mtaji na hivyo waachiwe walemavu wenyewe kuzishughulikia asasi
hizo kwa ustawi wa walemavu na kuondokana na kuwa ombaomba.
Aidha mchangiaji mwingine ametaka
walemavu wapate huduma za afya bure na suala hilo kuingizwa kwenye Katiba Mpya ambapo
akichangia kuhusiana na watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi ametaka Katiba
itamke kupata huduma za matibabu bure kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi.
Anapendekeza hukumu ya kifo ifutwe na
badala yake kuwepo na kifungo cha maisha jela ili kutoa nafasi kwa mkosaji
kujutia makosa yake akiwa gerezani badala ya kumhukumu kifo ambapo hata hivyo
katika utoaji wa mapendekezo hayo wajumbe walitofautiana katika kipengele hicho
ambapo wengine wametaka adhabu ya kifo ibaki kama
ilivyo.
Pia wachangiaji katika mkutano huo wa
Baraza la Katiba wametaka mawaziri wasiwe wabunge na kwamba wapewe nafasi hizo
kwa kuzingatia taaluma zao ili kuleta ufanisi katika utendaji wa kazi ambapo
akichangia katika hoja hiyo Bw.Selestine Mkomekwa ametaka Makatibu wakuu kwenye
Wizara kuwajibika.
Kat ika Baraza hi lo suala
lililochangiwa na wachangiaji wengi ni suala la Muungano huku wachangiaji wengi
wakipendekeza kuwepo na Muungano wa Serikali tatu na kubainisha kuwa Muungano
huo wa Serikali tatu utaondoa utata kwani rais wa Muungano atatatua kero zao
kwa kuwa wamekuwa wakinyanyasika.
Akichangia hoja kuhusiana na Muungano,
Mzee Daud Mtupa anasema kuwa nchi mbili Tanganyika
na Zanzibar baada ya kupata huru Tanganyika ilijipeleka jumla kwenye muungano na
kupotelea huko ambapo muungano wa sasa hauoneshi wameungana na nchi gani na
kupendekeza kurejeshwa kwa Serikali ya Tanganyika.
"Mimi napendekeza Tanganyika irudi kisha tuungane na napendekeza Zanzibar kuwe na Waziri Mkuu na Tanganyika kuwepo Waziri Mkuu na
kisha kuwepo na Rais wa Jamhuri ya Muungano ili kuondoa utata wa
kiutawala," alisema.
Mchangiaji mwingine ambaye ni mlemavu wa viungo Bw. Mngwali anazungumza
kwenye baraza hilo kuwa rasimu hiyo imekuja wakati mwafaka wa kudai Serikali ya
Tanganyika ambapo anapendekeza kuwepo na Serikali tatu, Serikali ya Muungano,
Tanganyika na Zanzibar na kwamba huenda akiwepo Rais wa Muungano atawajali
Walemavu.
Akichangia hoja
kwenye mkutano huo Bw. Percival Bwanali kwa upande wake anasema kuwa kwa kuwepo
na Muungano wa Serikali tatu kutaondoa utata wa Zanzibar
kujiona kuwa wanaonewa na Tanganyika.
Anasema kuwa kutokana na utata wa
muungano Wazanzibari wamekuwa wakidai nchi yao
kwa asilimia 100 hivyo muungano wa Serikali tatu utaondoa utata huu uliopo na
hivyo hakutakuwepo na malalamiko ya pande hizi mbili Tanganyika
na Zanzibar.
Kwa upande wake mshiriki Bw. Kasim
Lyanda anapendekeza kuwepo na Muungano wa Serikali tatu na kubainisha kuwa
kuwepo kwa Muungano huo kutaleta Muungano halisi kwa kuwa itaonesha Tanganyika imeungana na Zanzibar
tofauti na ilivyo sasa ambapo Serikali ya Tanganyika haipo.
Akichangia hoja kuhusiana na Muungano,
Bw. Mnung'a S. Mnug'a anasema kuwa Tanganyika na Zanzibar ni nchi zilizo huru
na hivyo zinaweza kuunda muungano wa Serikali tatu wenye rais mmoja na
akapendekeza kuwepo na magavana katika nchi za Tanganyika na Zanzibar na kubaki
na Rais mmoja wa Serikali ya Muungano.
No comments:
Post a Comment