UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Korogwe,
umewataka watendaji wa halmashauri kuweka utaratibu utakaowezesha vijana
kupatiwa mikopo itakayotokana na fedha zilizotengwa na Serikali kiasi cha
shilingi bilioni 6.1.
Mwenyekiti wa UVCCM wilayani Korogwe, Bendera Shekigenda alitoa
ushauri huo mwishoni mwa wiki kwenye mkutano wa siku moja kwa Saccos ya vijana
wa Korogwe vijijini ulioandaliwa kwa ajili ya kuwapatia mbinu vijana namna
watakavyojiandaa na mikopo hiyo.
Mkutano huo uliohusisha vikundi 169 vya vijana wanaounda Saccos
hiyo ambapo Shekigenda alisema ili waweze kunufaika na mikopo hiyo vijana
wanatakiwa kuwa wabunifu wa miradi wakijitahidi kutumia rasilimali walizonazo
na zilizowazunguka katika kuendesha miradi ya kujikwamua kiuchumi.
Alisema kwamba upatikanaji wa fedha hizo kama sehemu ya mikopo
kwao kutoka kwa Serikali yao inahitaji ubunifu wa hali ya juu kuwawezesha
kujikwamua kimaisha ambapo aliwasisitiza kuongeza ubunifu badala ya kufanya
biashara zitakazofanana utaratibu ambao unaweza kuwakwamisha.
Mbali na kuyasema hayo, Shekigenda pia aliwashauri maofisa wa
vijana kuwafikia vijana wote katika maeneo ya vijijini kuwaeleza juu ya fursa
iliyopo lengo likiwa kuwawezesha kushiriki katika mchakato wa kujiunga na
Saccos yao lengo likiwa kuwakwamua katika lindi la umaskini wa kipato kwa walio
wengi.
Mwenyekiti huyo alisema utolewaji wa mikopo hiyo unawahusisha
vijana wote bila ya kujali dini, itikadi za vyama vya siasa wala ukabila ambapo
aliwahimiza wajumbe wa mkutano huo kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao ambao
hawakuweza kupata taarifa ili waweze kuungana nao.
Kuhusu vikwazo ambavyo vitajitokeza wakati wa mchakato wa
upatikanaji wa mikopo, Shekigenda alisema kwamba ni vyema vijana watakaojihisi
kukwama kutokana na kujitokeza kwa upungufu mbalimbali wakajitahidi kuonana na
viongozi wao wakiwemo wale wa vijana ili kupatiwa ufumbuzi.
Katika mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Korogwe mkoani Tanga zaidi ya vijana 260 walihudhuria kutoka katika kata 12
ambapo walishiriki kuchangia rasimu ya katiba ya Saccos yao huku wakihimizwa
kuwa kwenye vikundi vya watu kuanzia idadi ya watano hadi kumi
No comments:
Post a Comment