Lilian Justice
Mizinga ya nyuki ikionekana pichani
ikiwa imetundikwa bila ya kuharibu mazingira. Picha na Lilian Justice
UHARIBIFU wa mazingira ni uzoroteshaji
wa mazingira kwa njia ya kupunguza rasilimali kama
vile hewa, maji na udongo.Kutokana na
uharibifu wa mazingira unaojitokeza kila mara katika maeneo mbalimbali ya nchi
yetu imepelekea Serikali kupitia Bunge kuanza kutunga sheria au kuweka mkakati
maalumu wa kuweza kuzuia uharibifu huo.
Uharibifu wa
mazingira unaofanywa na binadamu kutokana na kutafuta mahitaji yake unaweza
kudhibitiwa kwa njia mbalimbali kama kutakuwepo na ushirikiano mkubwa kati ya
Serikali na taasisi binafsi zinazopambana na utunzaji wa mazingira kila wilaya
na kila mkoa kwa elimu endelevu ya mazingira.
Katika Mkoa wa
Morogoro kuna tatizo kubwa la uharibifu wa mazingira japokuwa kuna taasisi
nyingi binafsi ikiwemo mashirika zinazopambana na changamoto hii inayochangia
mabadiliko makubwa ya tabia nchi yanatokea mara kwa mara kutokana na ukosefu
mkubwa wa elimu ya mazingira hasa katika Milima ya Uluguru.
Katika
kuhakikisha changamoto hiyo inavaliwa njuga taasisi isiyo ya kiserikali ya
Blesssing Group inayojishughulisha na ufugaji wa nyuki na samaki pasipo
kuharibu mazingira imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutekeleza majukumu yake
katika sehemu mbalimbali za Mkoa wa Morogoro za kuhimiza ufugaji salama ambao
haugusi mazingira.
Aidha
mwenyekiti wa asasi hiyo Aron Mlemi anaeleza kuwa malengo ya taasisi hiyo ni
kuinua uchumi, maendeleo ya wananchi sambamba na Mkakati wa Taifa wa Kukuza
Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA) pamoja na utunzaji wa mazingira
na misitu kwa kutoa elimu na upandaji wa miti sambamba na kutokata miti ovyo.
Anasema kuwa
asasi yao inatoa mafunzo kwa ajili ya kujenga uelewa kwa jamii na wadau wakuu
kushiriki katika ufugaji wa nyuki kitaalamu na utunzaji wa mazingira na
kuhamasisha kila kijiji katika wilaya ya Mvomero kutenga maeneo maalum kwa
kufanikisha mchakato huo.
Mlemi
anafafanua kuwa kupitia mradi wa ufugaji wa nyuki kwa njia bora ya kisasa
wamehamasisha kujenga uelewa kwa jamii kuonesha uthubutu kwani unasaidia katika
suala zima la utunzaji wa mazingira na kuongeza kipato katika jamii wanazoishi.
Vilevile
anaongeza kuwa kuanzisha na kuendeleza ufugaji wa nyuki kwa njia za kisasa wilayani
Mvomero unazingatia utunzaji wa mazingira na unaochangia kikamilifu kwenye
uchumi wa wafugaji pamoja na mradi huo.
Anataja malengo ya asasi kuwa ni
kuhamasisha ufugaji wa samaki, kuhimiza matumizi bora ya ardhi, matumizi bora
ya misitu na bionuwai, kuanzisha vitalu vya miti na mazao mengine rafiki wa
mazingira na nyuki, kilimo kinachochochea utunzaji wa mazingira kuhimiza
wafugaji wa nyuki kwamba ufugaji uwe wa kisasa na kuhimiza uzalishaji wenye
tija katika jamii.
Anasema kuwa kuna tatizo kubwa sugu
katika Wilaya Mvomero ya uchomaji wa misitu ovyo hasa nyakati za kiangazi,
maeneo mengi ya milimani yanakuwa tayari yameshawashwa moto kutokana na
shughuli za kilimo sababu kubwa ni kundi kubwa kuishi kwa kutegemea shughuli za
uchomaji mkaa kama njia ya kujipatia kipato na
hivyo kujikuta wanachangia kwa asilimia kubwa kuharibu mazingira.
Anasema kuwa asasi hiyo imejipanga
kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo Serikali katika
kuelimisha jamii umuhimu wa kutunza mazingira kwa kutambua miti na misitu ni
rafiki kwa binadamu na zawadi ya asili na faida nyingine kama mbao, asali na
anta, dawa za asili, malisho ya mifugo, hali ya hewa nzuri na yanzo vya maji.
Mwenyekiti huyo anasema kuwa kupita
mradi wa ufugaji wa nyuki asasi hiyo inaamini kuwa pamoja na kuongeza pato la
taifa na kaya kwa kiasi kikubwa pia inasaidia kulinda misitu na utunzaji wa
mazingira kwa faida ya vizazi vilivyopo na vizazi vijavyo kwani mazingira
mazuri ndiyo yatachangia kuwepo kwa huduma hizo muhimu ndani ya jamii.
Wafugaji wengi wa nyuki wakihamasishwa
katika kila kijiji na kutenga maeneo wanajikuta wameingia katika utunzaji wa
mazingira kwani bila miti huwezi kufuga nyuki na watakosa chakula kwani nyuki
wanategemea kwa asilimia kubwa kupata vyakula vyao katika miti.
Katika mchakato mzima wa ufugaji wa
nyuki hakuna mfugaji anayekubali shamba lake la mizinga likachomwa moto na
jamii ikiwa na uelewa umuhimu wa misitu itasaidia katika kulinda na kutunza
mazingira kwa kuwa wanaelewa tayari faida wanayoipata kutokana na kuweka mazingira
katika hali ya usalama.
Anasema kuwa changamoto zinazojitokeza
katika suala zima la ufugaji wa nyuki kwa njia za kisasa na utunzaji wa
mazingira ni kutokuwa na elimu endelevu ya ufugaji wa nyuki kitaalamu kwa njia
bora za kisasa badala ya ufugaji uliojengeka wa mizinga ya magome ya magogo
ambao huchangia kwa asilimia kubwa uharibifu wa mazingira.
Anasema kuwa nyingine ni pamoja na
asali kuuzwa kabla ya kuchakatwa wilayani Mvomero na mwingiliano mkubwa wa
matumizi ya ardhi ambayo si rafiki kwa ufugaji nyuki kwa bora ya kisasa, nyuki
kuhama kwa kukosa chakula kwa tatizo la uchomaji moto misitu ovyo, ukosefu wa
vitendea kazi, ukosefu wa rasilimali fedha na mwamko mdogo katika ufugaji wa
nyuki.
Kutokana na jitihada zinazofanywa na
asasi, serikali wilayani Mvomero kupitia Mkuu wa Wilaya, Antony Mtaka wakati
anazungumza na vikundi vinavyojihusisha na ufugaji wa nyuki na utunzaji
mazingira kutoka Tarafa ya Turiani anasema kuwa Serikali itaendelea
kushirikiana na taasisi hiyo katika harakati za kuleta maendeleo hasa katika
nyanja za utunzaji wa mazingira ambayo imekuwa kero kubwa kwa taifa.
Mtaka anabainisha kuwa mchango
unafanywa na taasisi binafsi hasa zinazopambana na mazingira katika kuleta
maendeleo ni mkubwa sana na Serikali inathamini sana mchango wao na watakuwa
mstari wa mbele katika kuhakikisha zinakabiliana na changamoto zinazoikabili
jamii kwa nyakati taofuti.
“Sisi Serikali tutakuwa mstari wa mbele
katika kutoa mchango wetu kwa taasisi binafsi hasa zile zinazopambana na
utunzaji wa mazingira kwani uharibifu wa mazingira unachangia mabadiliko
makubwa ya tabia ya nchi,” alisema Mtaka.
Anaeleza kuwa ufugaji wa nyuki hauna
gharama kubwa ila kinachotakiwa ni mfugaji kuwa na elimu ya kutosha na kufuata
mbinu sahihi za ufagaji kwa lengo la kupata mazao bora pasipo kuharibu
mazingira kwa kuchomo moto misitu ya asili ambayo ni kivutio katika jamii.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa
ufugaji nyuki kwa njia za kisasa na utunzaji wa mazingira, Richard Haule,
anasema kuwa asasi imejikita katika mradi wa ufugaji nyuki kama chanzo kikuu
cha mapato na kushiriki kikamilifu vikundi ambao ni wadau wakuu wa maendeleo
katika jamii kwa kadiri ya fursa kwa kufuga na kutunza mazingira kwa
kushirikiana na Serikali kama mdau mkubwa wa maendeleo ya umma.
Haule anasema asasi inatoa elimu kwa
jamii na kujenga uelewa kupitia vikundi mbalimbali vya kijamii kuamsha na
kushirikisha kikamilifu katika mradi wa ufugaji wa nyuki kwa njia bora ya
kisasa na utunzaji wa misitu ya kupandwa na misitu asili pia ufugaji wa samaki
ikiwa ni jitihada za kupambana na umaskini katika jamii.
Naye mmoja wa wafugaji wa nyuki Katika
Wilaya ya Mvomero, Msafiri Kimath anasema kuwa ufugaji wa nyuki unaweza
kumkwamua mwananchi kiuchumi na kuweza kutatua changamoto mbalimbali za
kimaisha ikiwemo kusomesha watoto ,ujenzi wa nyumba ya kuishi na hata kuweza
kumudu gharama mbalimbali za matibabu kwa familia.
Kimath anasema kuwa ni vyema wananchi
wakaachana na kasumba kuwa ufugaji wa nyuki hauna tija kwa maendeleo jambo
ambalo si sahihi na badala yake wananchi wanaotaka kujikita katika ufugaji wa
nyuki kuwasiliana na maafisa ugani ili waweze kuwapa elimu juu ya ufugaji bora
wa kisasa wa nyuki.
Hivi karibuni Waziri Mkuu Mizengo Pinda
alitoa tamko kuwa Serikali iko mbioni kuanzisha chuo maalum kwa ajili ya kutoa
mafunzo ya ufugaji bora wa nyuki ikiwa ni lengo la kuhakikisha sekta ya misitu
na nyuki inakuwa kwa kasi na kuweza kumletea tija mwananchi.
Hata hivyo ili Serikali iweze kufikia malengo
hayo ni vyema ikahakikisha maofisa ugani wanawafikia wananchi katika maeneo ya
vijijini kwani ndiko kuliko na wananchi wengi ambao bado hawana uelewa mkubwa
juu ya ufugaji wa nyuki jambo ambalo linawapelekea baadhi yao kujikuta
wakiharibu mazingira huku baadhi yao wakikumbwa na ulipaji wa fidia kutokana na
uharibifu huo
No comments:
Post a Comment