24 September 2013

TOP LAND WATWAA UBINGWA WA POOL TAIFA Na Mwandishi Wetu. Morogoro
    Klabu ya Top Land kutoka mkoa wa kimichezo wa Kinondoni jijini Dar es Salaam wameibuka mabingwa katika fainali za kitaifa za mashindano ya Safari Pool 2013, yaliyomalizika mwishoni mwa wiki mkoani Morogoro.

Top Land walitwaa ubingwa huo kwa kuifunga klabu ya Mpo Afrika ya Temeke 13-10 na hivyo kuzawadiwa fedha taslimu sh. 5,000,000, kikombe na medali za dhahabu kwa kila mchezaji.Mshindi wa pili katika fainali hizo ni klabu ya Mpo Afrika ambayo ilizawadiwa fedha taslimu sh. 2,500,000 na medali za fedha kwa kila mchezaji.
Mshindi wa tatu ni klabu ya Supersport kutoka Mkoa wa Manyara ambao walizawadiwa fedha taslimu sh. 1,250,000 na medali za shaba na mshindi wa nne ni klabu ya Mashujaa kutoka mkoa wa kimichezo wa Ilala ambao walizawadiwa fedha taslimu sh. 1,000,000.
Upande wa mchezaji mmoja mmoja wanaume(singles), mchezaji Festo Yohana kutoka klabu ya Mashujaa ya mkoa wa kimichezo wa Ilala alitwaa ubingwa wa Taifa kwa kumfunga Mussa Mkwega kutoka Morogoro 5-1 na kuzawadiwa fedha taslimu sh. 700,000, kikombe na medali ya dhahabu ambapo mshindi wa pili ni Mussa Mkwega ambaye alijinyakulia fedha taslimu sh. 350,000 na medali ya Fedha.
Mshindi wa tatu ni Mohamed Idd kutoka klabu ya Atlantic ya mkoani Dodoma ambaye alizawadiwa sh. 200,000 na medali ya shaba ambapo mshindi wa nne ni Ernest John kutoka Tabora ambaye alizawadiwa sh. 150,000.
  Upande wa mchezaji mmoja mmoja wanawake(Singles), mchezaji Rose Deus kutoka Mkoa wa Morogoro alitwaa ubingwa wa kitaifa kwa kumfunga Cecilia Kileo kutoka Ilala 5-4 na hivyo Rose kuzawadiwa fedha taslimu sh. 350,000, Kikombe na medali ya dhahabu ambapo Cecilia alikamata nafasi ya pili na kuzawadiwa sh. 200,000 na medali ya fedha.
   Nafasi ya tatu ilichukuliwa na mchezaji Merry Gumbu kutoka Arusha ambaye alizawadiwa sh.150,000 na medali ya shaba na nafasi ya nne ilichukuliwa na Judith Machafuko kutoka mkoa wa Kinondoni ambaye alizawadiwa sh. 100,000.
   Fainali hizo za kitaifa zilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Utamaduni ,Vijana  na Michezo, Amos Makalla ambaye alikipongeza Chama cha Pool Taifa (TAPA), kwa kuufikisha mchezo hapo ulipo ambapo mpaka sasa umesambaa katika mikoa 17 ambayo ilishiriki mashindano hayo na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kama serikali kwa kuutambua na kutoa msaada watakapohitaji.
   Makala pia aliipongeza TBL kupitia Bia ya Safari Lager kwa kuendelea kudhamini mchezo wa Pool kwa mwaka wa sita sasa na kuwaomba waendelee kudhamini kwa miaka ijayo. Lakini pia alimpongeza Meneja wa Bia ya Safari Lager,Oscar Shelukindo kwa Brand yake ya Safari kuwa bia namba moja Afrika na kumwomba aendelee kudhamini Pool ikamate namba moja katika mashindano ya Pool ya Afrika yanayotarajiwa kufanyika Malawi hivi karibuni.

No comments:

Post a Comment