30 September 2013

SIMBA YAENDELEZA WIMBI LA USHINDI



Na Speciroza Joseph
Timu  Simba jana iliendeleza wimbi la ushindi baada ya kuinyuka JKT Ruvu Mabao 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mpira ulianza kwa timu zote kucheza kwa kusoma mchezo ambapo dakika ya tatu, Abdulhalim Humud aliikosesha Simba bao baada ya kupata nafasi nzuri lakini shuti lake likatoka nje ya uwanja.Dakika ya saba Amis Tambwe, akiwa katika nafasi nzuri alishindwa kuunganisha krosi safi ilichongwa na kiungo Amri Kiemba ambapo kipa wa JKT, Shaban Dihile aliuwahi na kuudaka.
Baada ya kosakosa hizo JKT iliamka dakika ya 18 na kufanya shambulizi langoni mwa Simba lakini, Salum Machaku badala ya kufunga akapiga shuti liliotoka nje ya lango.JKT Ruvu ililifuata tena lango la Simba dakika ya 20 ambapo Damas Makwaya, aliachia shuti kali lililodakwa na kipa Abel Dhaira.
Simba ilipata bao la kwanza dakika ya 24 kwa mkwaju wa penalti uliokwamishwa wavuni na Tambwe baada ya mabeki wa JKT kufanya madhambi katika eneo la penalti, lakini wachezaji na viongozi wa ‘maafande’ hao walikuja juu kupinga adhabu hiyo ambayo hata hivyo mwamuzi aliamuru ipigwe.
  Dakika ya 45 Ramadhan Singano, aliikosesha Simba bao akiwa na lango lakini shuti lake likatoka nje ya lango. Huku Haruna Chanongo naye akikosa bao la wazi baada ya kupiga shuti lililotoka nje ya lango.Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo dakiak ya 40, Daniel Pius wa JKT Ruvu kupiga mpira wa kichwa ambao hata hivyo ulitoka nje ya lango.
  Simba ilipata bao la pili dakika ya 50 kupitia kwa Singano kwa shuti akiunganisha pasi nzuri ya Humud.Dakika ya 60 Bakari Kondo wa JKT aliikosesha timu yake bao baada ya kubaki na nyavu lakini shuti lake likatoka nje ya lango, huku Amos Mgisa naye akiikosesha timu hiyo bao dakika ya 67 baada shuti lake kudakwa na kipa Dhaira.
  JKT Ruvu walikosa bao la wazi dakika ya 89 baada ya Kondo ambaye alikuwa katika nafasi nzuri kupiga mpira mrefu uliotoka nje kidogo ya lango la Simba.Katika mechi nyingine, Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya Azam FC ilitoka sare ya bao 1-1 na Prisons, bao la Azam likifungwa na Kipre Tchetche dakika ya 49 huku la Prisons likiwekwa kimiani na Peter Michael dakika ya 36.
  Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Ashanti United ilitoka sare ya mabao 2-2 na Mtibwa Sugar. Mabao ya Ashanti yalifungwa na Paul Maone na Tumba Swedi, huku ya Mtibwa yakitumbukizwa na Shaaban Kisiga.

No comments:

Post a Comment