30 September 2013

JK AKOSOA UTENDAJI ICCNa Mwandishi Wetu
  Rais Jakaya Kikwete, amesema mwenendo wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), kuhusu Bara la Afrika na viongozi wake, unainyima mahakama hiyo nafasi kubwa ya kuungwa mkono barani Afrika
. Alisema kuanzishwa kwa ICC kumetokana na Mkataba wa Rome ambao ulikuwa ni hatua muhimu katika mfumo wa kimataifa kupambana na makosa ya jinai.Rais Kikwete alitoa msimamo huo mwishoni mwa wiki wakati akilihutubia Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA), katika Makao Makuu ya umoja huo, New York, Marekani.
Katika hotuba yake, Rais Kikwete pia alilaani mashambulizi yanayoongezeka dhidi ya vikosi vya kimataifa vya kulinda amani katika nchi mbalimbali duniani vikiwemo kutoka Tanzania."Kwa hakika, kuundwa kwa mahakama hii kuliweka mfumo mzuri wa kuondokana na watu kutenda vitendo vya jinai, hata hivyo mwongo mmoja baada ya kuanzishwa mahakama hii, mvutano umezuka kati ya ICC na Bara la Afrika.
"Sasa mahakama hii inaonekana kama taasisi isiyojali maoni na msimamo wa Afrika kwa mambo ambayo kwa maoni yangu ni hofu halali ya Waafrika," alisema Rais Kikwete.Aliongeza kuwa, bado mahakama hiyo inaendelea kupuuza maombi ya mara kwa mara ya Umoja wa Afrika, hivyo ni jambo la kutia huzuni kuwa maombi ya kubadilisha muda wa kuanza kusikilizwa kwa kesi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya; na Naibu Rais William Ruto yalipuuzwa na hayakujibiwa.
"Tabia hii imekuwa ni tatizo kubwa linaloleta kikwazo kwa ICC kushindwa kutimiza wajibu wake wa kupambana na tabia ya watu wanaofanya makosa ya jinai kutokuchukuliwa hatua."Kwa hakika, kugangamara kwa ICC hata katika masuala yaliyo wazi, kumethibitika kuwa kunainyima mahakama hii nafasi ya kuendelea kuungwa mkono Barani Afrika," alisema.
Rais alisema Tanzania ni moja ya nchi zinazoshiriki shughuli za kimataifa za kulinda amani chini ya Umoja wa Mataifa ikiwa na zaidi ya walinda amani 2,500 Darfur, nchini Sudan, Lebanon na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Alisema Tanzania ni nchi ya sita katika Afrika na 12 duniani kwa kutoa walinzi wa amani duniani ikiridhishwa na mchango mdogo wanaoutoa katika shughuli hiyo.Aliongeza kuwa, wakati mwingine Tanzania inalipa gharama kubwa na maisha ya vijana wake katika shughuli hizi kama ilivyotokea Darfur na DRC ambapo askari wake ambao ni walinda amani walipoteza maisha. Rais Kikwete alikuwa katika ziara ya kikazi nchini Marekani na Canada na atarejea nchini leo.

No comments:

Post a Comment