Na Martha Fataely, Moshi
HALI
ya taharuki na simanzi jana vilitawala katika Mahakama ya Kakimu mkazi mjini
Moshi wakati wa kesi ya watuhumiwa wa mauaji ya mfanyabiashara wa Arusha,
Erasto Msuya baada ya ndugu wa marehemu kuangua vilio na wengine kupoteza
fahamu kwa muda.
Tukio hilo
linafuatia wanandugu hao kuwaona washtakiwa katika kesi hiyo ambayo
iliahirishwa hadi Septemba 18, mwaka huu kutokana na kutokamilika kwa upelelezi
wake.Wanandugu ambao
ni dada wa marehemu Msuya, Antuja Msuya na Bahati Msuya, ambao waliangua vilio
huku wakidai kaka yao ameuawa kikatili pia walianguka chini na kupoteza fahamu
ingawa waliondolewa na kupelekwa katika magari ya ndugu wengine waliokuwepo.
Pamoja na hilo lakini pia Jeshi la
Polisi kutokana na umati wa wakazi wa manispaa hiyo walifurika mahakamani hapo,
liliimarisha ulinzi kwa kutumia askari kanzu, wale wa kutuliza ghasia (FFU),
askari wa pikipiki na kikosi maalum cha kupambana na majambazi wote wakiwa na
silaha.
Awali mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama
hiyo, Theotimus Swai,wakili wa Serikali, Stella Majaliwa aliieleza mahakama
kuwa mshtakiwa wa pili, Shaibu Mpungi hakufika mahakamani hapo kutokana na
kusumbuliwa na maradhi ingawa hakuyabainisha.Wakili Majaliwa aliieleza mahakama hiyo
kuwa anaomba kuahirishwa kwa kesi hiyo kutokana na kutokamilika kwa upelelezi
wa shauri hilo.
Naye wakili wa utetezi anayewatetea
mshtakiwa wa kwanza Sharifu Mohamed na wa tatu Musa Mangu, aliuomba upande wa
mashtaka kuharakisha upelelezi ili kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo mapema.Akiahirisha kesi hiyo,hakimu mkazi wa
mahakama hiyo, Swai alisema maombi ya upande wa utetezi yamesikika na upande wa
mashtaka na hivyo kutaka washtakiwa hao kurudi rumande hadi Septemba 18, mwaka
huu.
Kesi hiyo ilifikishwa mahakamani hapo
Agosti 21 mwaka huu, ambapo watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kuua kwa
kukusudia mfanyabiashara wa madini, Msuya kwa kumpiga risasi.Mfanyabiashara huyo aliuawa Agosti 7 mwaka huu saa 6:30 mchana kwa
kupigwa risasi 13 kifuani, kando ya barabara kuu ya Arusha - Moshi katika eneo
la Mjohoroni, Wilaya ya Hai, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Kilimanjaro (KIA).
No comments:
Post a Comment