Na Salim Nyomolelo
WAZIRI
wa Afya Dkt. H u s s e i n M w i n y i amezindua kipimo cha malaria kinachotoa
majibu ya haraka (mRDT) katika vituo binafsi vya kutolea huduma za afya huku
akisisitiza wananchi kupima kabla ya kumeza dawa.
Akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam jana mara baada ya kuzindua kipimo hicho Dkt.
Mwinyi alisema kuwa asilimia 40 ya Watanzania wanatibiwa katika vituo binafsi
vya kutolea huduma za afya na hivyo ni vyema kipimo hicho kikatumika pamoja na
vituo hivyo.
Alisema kuwa mRDT itasaidia kutoa
majibu ya haraka na kuthibitisha kama mgonjwa ana ugonjwa wa malaria kwa vituo
ambavyo havina huduma za maabara.Alisema kuwa utafiti katika jamii kwa
muda wa miaka mitano unaonesha kuwa maambukizo ya ugonjwa wa malaria yamepungua
kwa zaidi ya asilimia 50 kutoka asilimia 18 mwaka 2007 hadi kufikia asilimia 9
mwaka jana.
“Kutokana na kazi nzuri ya kupambana na
ugonjwa wa malaria, tumepata mafanikio makubwa na kiasi cha maambukizo
kimepungua na wizara inasisitiza kutumia mkakati mpya wa kupima kabla ya
kutumia dawa na kujua ni ugonjwa gani unakusumbua,” alisema Dkt. Mwinyi
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tiba
Wizara ya Afya, Magreth Mhando alisema kuwa mRTD ni kipimo cha haraka cha
kutambua malaria na cha kuaminika ambapo kinatoa majibu kuanzia dakika 15 hadi
20 ya kuwepo ama kutokuwepo kwa vimelea vya malaria.Hata hivyo Mhando alisema kuwa alama ya kipimo hicho ni nembo ya V ya
rangi ya bluu na vinapatikana kwa bei nafuu.
No comments:
Post a Comment