Na Mwajuma Juma, Zanzibar
Chama cha Wananchi (CUF) kimemtaka
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd,
kujiuzulu wadhifa huo kwa kushindwa kusimamia maslahi ya Zanzibar.
Kauli hiyo
ilitolewa mjini Zanzibar jana na Mjumbe wa Baraza Kuu la CUF, Ismail Chusa
Razu, wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Kibanda
Maiti.
Alisema Balozi
Seif amegeuka dalali wa kuiuza Zanzibar baada ya kukiri kuwa Zanzibar
ilishirikishwa katika Mswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Muungano
katika kipengele kinachohusu Zanzibar, jambo ambalo sio kweli.
Aliongeza kuwa,
Balozi Seif akiwa kiongozi alistahili kuzungumza na Waziri wa Katiba na Sheria
pamoja na Mwanasheria Mkuu ndipo apate cha kuzungumza.
"Namtaka
Balozi Seif ajiuzulu nafasi yake kwa kushindwa kusimamia maslahi ya Zanzibar,
ikiwa ana uchungu wa Zanzibar hakustahili kusema hivyo," alisema na
kuongeza kuwa kuanzia sasa watakuwa wakimuita Balozi Mkazi wa Tanganyika na
Zanzibar.
Kwa upande wa
kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru,kusema anashangaa wazee wenzake
kuleta rasimu ya Serikali tatu wakati Serikali mbili zilizopo kila moja ina
mipaka yake na Zanzibar na bara zilikufa mwaka 1964 wakati nchi mbili
zilipoungana,Chusa alisema Zanzibar bado ipo hai na itaendelea kuwa hai hadi
kiama.
Alisema iliyokufa ni Tanganyika hivyo
kama lengo ni kuizika Zanzibar bado hawajafanikiwa kwani Wazanzibari wapo
macho."Zanzibar ipo hai na itaendelea
kuwa hai hadi kiama, nchi hii haijazikwa," alisisitiza.
Kwa upande wake Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad, alimtaka
Rais Jakaya Kikwete, asisaini mswada huo, kwani ana nia nzuri, lakini wenzake
wanataka kumpeleka kubaya.
"Rais Kikwete ana nia nzuri lakini
wenzako wanakupotosha, usisaini mswada huu tunajua una nia nzuri,"alisema
Maalim Seif na kuongeza kuwa iwapo atakubali kusaini mswada huo atazuia wajumbe
wa chama hicho wasishiriki Bunge la Katiba.
Alishauri mswada huo urejeshwe Zanzibar
ili kupata Katiba Bora. Kuhusu Balozi Seif, Maalim Seif alisema anamuonea
huruma makamu mwenzake huyo kwa sababu hakujua ni mswada upi aliuona.
Alisema Mei 6, mwaka huu aliitwa Dodoma
na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kuambiwa kuwa wanataka kufanya marekebisho
kwenye vipengele sita ambapo walifanya marekebisho, lakini waliporudi Tanzania
Bara walifanya marekebisho kwenye vipengele nane.
Alisema makamu wake hakujua hilo na
anashangaa ni kwa nini wana-CCM wenzake wamemtosa. Alisema bila shaka walikuwa
wamepanga jambo hilo.Alisema Waziri wa Sheria na Katiba Zanzibar, Mwanasheria
Mkuu, Rais wa Zanzibar na yeye mwenyewe hawakubaliani na hilo.
No comments:
Post a Comment