19 September 2013

SHAHIDI KESI YA MRAMBA AMTWISHA ZIGO BALALI Na Rehema Mohamed

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Masoko na Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Kesisia Mbatia, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa benki hiyo ilihusika katika mchakato mzima wa kumtafuta mzabuni wa ukaguzi wa madini ya dhahabu nchini ambaye ni Kampuni ya M/S Alex Stewart ya nchini Uingereza.

Mbatia alieleza hayo jana mahakamani hapo wakati akitoa ushahidi wake mbele ya Jopo la Mahakimu wawili wakiongozwa na Jaji John Utamwa, waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha Basil Mramba na wenzake.

Mbatia alisema kuwa katika mchakato wa kumtafuta mzabuni huyo, aliyekuwa Gavana wa BoT, marehemu Daud Balali, alimteua yeye kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wajumbe watano wa kutafuta mzabuni huyo.

Alidai kuwa, awali jumla ya wazabuni 21 walijitokeza kutaka kufanya kazi ya ukaguzi huo na baadaye walifanya mchujo na kubaki na wazabuni watano, ambapo kati ya hao ni Kampuni ya M/S Alex Stewart ndiyo ilishinda.

Alisema kampuni hiyo ilishinda zabuni hiyo kwa makubaliano ya kulipwa asilimia 1.9 ya dhahabu atakayokagua na kwamba asingehusika na malipo yoyote ya kodi za hapa nchini.

Alidai kuwa baada ya kushinda dhabuni hiyo,BoT iliandaa rasimu ya mkataba kati ya Serikali na M/S Alex Stewart ambapo Balali alimwalika kuja nchini kwa ajili ya kusaini mkataba huo ambapo kwa upande wa Tanzania Balali ndiye aliyesaini.

Aliongeza kuwa mkataba huo ulikuwa wa kufanya kazi miaka miwili na baada ya muda huo kumalizika, Balali ilimwandikia barua M/S Alex Stewart kuongeza muda wa miaka miwili mingine ya kufanya kazi hiyo.

"Kampuni ya M/S Alex Stewart iliongezewa mkataba Machi 2005, kipindi hicho Kamishna wa Madini ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa kamati na hatukuwa na kazi kubwa kama awali kwani barua aliyoandikiwa na Balali ilimaliza kila kitu," alidai Mbatia.

Alidai kuwa walichojadili wao katika mkataba wa pili ni kuitaka kampuni hiyo kupanua zaidi kazi yake na kwamba hakumbuki kitu ambacho kiliongezwa na kama Mramba alihusika kwa namna yoyote katika kamati ya kutafuta mzabuni huyo.

Mbali na Mramba wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja.

Katika kesi hiyo ambayo itaendelea kusikilizwa leo, Mramba na wenzake wanashtakiwa, wakidaiwa kwamba kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14, 2004, jijini Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma walitumia vibaya madaraka yao na kuisababishia Serikali hasara ya Sh.bilioni 11.7.


1 comment:

  1. SI MNAONAAAAA!!!!!! UKIZUBAAA KIDOGO TU UNAKATWA KIDIZAINI FULANI.

    ReplyDelete