Na Goodluck Hongo
MSWADA wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
umezidi kugeuka kaa la moto kutokana na kuongezeka kwa shinikizo kutoka kwa
watu na taasisi mbalimbali wanaomtaka Rais Jakaya Kikwete, asisaini mswada huo
ili kuwa sheria kwa kile kinachodaiwa kuwa ulipitishwa kiujanjaujanja.
Ili kuhakikisha
muswada huo hausainiwi, vyama vitatu vilivyoungana kupinga mchakato wa Katiba
Mpya vya CHADEMA, NCCR-Mageuzi na CUF vimezidi kutafuta nguvu ya kuungwa mkono
kwa kukutana na makundi mbalimbali ndani ya jamii kwa lengo la kuunganisha
sauti ili kukwamisha mswada huo.
Jana, viongozi
wa vyama hivyo, Freeman Mbowe (CHADEMA), Prof. Ibrahim Lipumba (CUF) na James
Mbatia (NCCR-Mageuzi) walikutana na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Watu
Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVIWATA) na kuwaeleza kasoro zilizoko kwenye mswada
huo kwa lengo la kutaka kuungwa mkono.
Mazungumzo ya viongozi hao na SHIVIWATA
yalifanyika jana asubuhi na baada ya kumalizika wanasiasa hao waliendelea na
ratiba yao ya kukutana na vyama vingine vya walemavu vidogo vidogo Makao Makuu
ya CUF, Buguruni, jijini Dar es Salaam.
Mikutano hiyo ya vyama hivyo vitatu vya
siasa ni mwendelezo wa mikutano mingine ambayo tayari imeishafanyika tangu
wabunge wake wasusie mjadala wa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba
Mpya.
Tangu kumalizika kwa Bunge, vyama hivyo
vimeshafanya mikutano na Jukwaa la Wahariri Tanzania, Jukwaa la Katiba na
SHIVIWATA; na Jumamosi vitafanya mkutano mkubwa viwanja vya Jangwani ili
kueleza jinsi mswada huo ulivyopitishwa kiujanja ujanja.
Wakati hayo yakiendelea wadau
mbalimbali wameshauri mswada huo usithubutu kupelekwa Ikulu kwa Rais Kikwete
ili ukasainiwe na kuwa sheria.Wakizungumza Dar es Salaam jana wakati
wa mjadala wa wazi wa nini kifanyike hadi sasa mchakato wa mabadiliko ya katiba
ulipofikia, wadau hao walisema yanatakiwa yafanyike maombi ya kukwamisha mswada
huo.
Mjadala huo ulioandaliwa na mtandao wa
jinsia (TGNP). Mwenyekiti wa Jukwaa la katiba, Deus Kibamba, alisema mchakato
wa mabadiliko ya Katiba haukuanza kwa huruma ya Rais Kikwete, bali watu
waliudai kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita, hivyo inabidi ufanyike kwa uwazi.
Alisema huo ni mchakato wa kwanza
kufanyika kwa wananchi kutoa maoni yao, lakini umeanza kutushinda kutokana na
wananchi kukosa elimu ya katiba.Aliyekuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, Dkt. Xavery Rweitama, alisema mjadala wa mswada huo umetekwa na
wanasiasa jambo ambalo limekuwa mwiba mkali kwao.
Alisema kuna wanasiasa wa ajira na wale
ambao wanataka masilahi ya wananchi. Alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba
imetokana na shinikizo la nje ya bunge ndiyo maana imeweza kufanya mambo mazuri
ikiwa ni pamoja na kupendekeza Serikali tatu.Alisema suala la Serikali tatu limekuwa
mwiba mkubwa kwa CCM kutokana na chama hicho kuamini kuwa kinaweza kutawala
milele.
Naye Mwakilishi Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC) Anna Henga, alisema kwa sasa kuna hali ya wanasiasa
kuteka machakato wa katiba kwani wananchi wamebaki kuzungumzia Serikali tatu
tu.Alisema
ni lazima wananchi wajue kutenganisha siasa na Katiba Mpya, kwani walio wengi
wanaamini kuwa wahusika wakuu ni wanasiasa na si wananchi.
Kaa la moto kwa nani? Mnajidanganya kama sio wasomi? Upinzani hauna uwezo wa kuzuia mswada wowote kama demokrasia inatumika bungeni. Wasomi wanaelewa hivyo. Wasaidieni upinzani kupata majority bungeni kwa njia halali ili waingize agenda zao wanazotaka. Kwa sasa haiwezekani kama kweli bunge linaendeshwa kwa utashi wa kidemkrasia na kupiga kura.
ReplyDeletePia muelewe wananchi wa kawaida hawaelewi hoja mnazopigania! wanshabikia tu kwamba "Sugu bwana kampiga ngumi askari" basi. Msitegemee nguvu ya umma kumng'oa JK mnaota ndoto za mchana
Jk anapendwa na wananchi wengi wa kawaida. Anafanya kazi kwa uangalifu sana wala sio kwa jazba!