02 September 2013

KATIBA MPYA ISIWANUFAISHE WANASIASA - SHIBUDA



 Na Suleiman Abeid, Simiyu
MBUNGE wa Maswa Magharibi, mkoani S imi y u , Bw. J o h n Shibuda (CHADEMA), amewataka Watanzania kuhakikisha Katiba Mpya nayo inatambua masilahi, maendeleo yao na kuzingatia misingi ya utawala bora badala ya kuwanufaisha wanasiasa wenye malengo binafsi
.Bw. Shibuda aliyasema hayo juzi wakati akiwahutubia wananchi kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya makumbusho ya mila za Kisukuma yaliyofanyika katika Mji wa Malampaka, wilayani humo.
Alisema wananchi wanapaswa kutambua kuwa, katiba ya nchi yoyote duniani ndiyo wokovu wa uhuru, maendeleo hai ya jamii husika na Taifa ambapo kama Watanzania watazembea na kusababisha kupatikana kwa katiba mbovu, watakuwa wamejiwekea tanuri la kukaushia haki zao.
Aliongeza kuwa, ni muhimu wakawa watulivu, kusoma taswira na mazingira ya kila hatua juu ya msukumo wa maoni yanayotolewa na makundi mbalimbali kuhusu katiba ijayo iwe na mfumo gani.
"Tupatapo mawazo ya rasimu toleo la pili, tuhakikishe tunatafakari na kusemezana kwa madhumuni ya kupata katiba bora itakayobeba masilahi ya wananchi, tuhakikishe tunapata Katiba Mpya ambayo itaendeleza umoja wetu wa kitaifa.
"Katiba ijayo ing'arishe palipotokea uchakavu wa masilahi ya jamii na Taifa, Katiba Mpya iwe nguzo kuu ya kusimamia ustawi na maendeleo ya uongozi wa kidemokrasia inayotoa fursa za utawala bora dhidi ya dhuluma kwa jamii," alisema.
Bw. Shibuda alisema katiba inayohitajika kwa Watanzania iwe mlango wa dira ya kujengwa maisha bora ya wafugaji, wakulima, wavuvi, watumishi wa sekta ya umma, binafsi na kuiwezesha nchi kupata viongozi bora.
"Tuwe makini ili tusipate katiba ambayo ni malighafi ya maisha bora kwa nchi za Ulaya na Watanzania kugeuzwa vibarua na watumwa wa utandawazi kupitia rasilimali zetu," alisema

No comments:

Post a Comment