Na
Mwandishi Wetu
Operesheni Kimbunga ya kuwaondoa
wahamiaji haramu nchini imezidi kuibua mambo mapya kutokana na kukamatwa kwa
watuhumiwa wa ujambazi wa kutumia silaha 55, mabomu ya kurusha kwa mkono
manane, bunduki 47
. Taarifa
iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana Kiongozi wa Timu ya Habari na
Mawasiliano ya Operesheni Kimbunga, Zamaradi Kawawa, juzi ilieleza kuwa
watuhumiwa hao wamekamatwa kuanzia Septemba 6, 2013 hadi kufikia Septemba 17,
2013.
Alisema
miongoni mwa silaha zilizokamatwa katika operesheni hiyo ni bunduki aina ya SMG
(4) Shotgun (4) Riffle (2) Mark IV (1) na Gobori 37.Alisema risasi
602 zilikamatwa zikiwemo risasi 500 za bunduki ya aina ya SMG na SAR, risasi
(20) za bunduki aina ya Mark IV na risasi (82) za bunduki aina ya Gobori, fataki
(8), mitambo ya kutengeneza magobori (2), misumeno ya kukata miti (9), mbao
(1,516), magogo (86), na mkaa magunia (111).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo tangu kuanza
kwa Operesheni hiyo ya kuwaondoa kwa lazima imefanikiwa kuwahamisha nchini
wahamiaji haramu 7,819.Aliongeza kuwa watendaji wa Operesheni
Kimbunga pia wamefanikiwa kukamata majangili Watanzania watatu, vipande vya
meno ya tembo (2), pamoja na ngozi za wanyama mbalimbali..
Wakati huo huo, ng'ombe
3,436 wamekamatwa baada ya wafugaji haramu kutelekeza mifugo hiyo wakati
walipozingirwa na timu ya operesheni kimbunga katika mikoa ya Kagera, Kigoma na
Geita."Kumekuwepo na tabia ya baadhi ya
wamiliki wa mifugo kutoka nchi jirani ambao wengi wao ni matajiri na viongozi
Serikalini kuwatuma watumishi wao kuingiza mifugo katika ardhi ya Tanzania
hususan kwenye hifadhi ya Taifa kwa ajili ya malisho na watumishi hao hupewa
silaha kwa ajili ya kujihami wakiwa kazini," alisema Zamaradi na kuongeza;
"Operesheni Kimbunga
itahakikisha inawakamata wahalifu wote wanaotishia amani hususan katika mikoa
ya Kagera, Kigoma na Geita."Alisema wananchi ambao ni raia pamoja
na raia wenye asili ya nchi jirani wanaowakaribisha na kuwahifadhi wahalifu na
wahamiaji haramu watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Operesheni Kimbunga inayoongozwa na Brigedia Jenerali Mathew
Sukambi imeanza rasmi Septemba 6, 2013 baada ya kutoa muda wa wiki mbili kwa
wahamiaji wanaoishi nchini bila kufuata sheria kuondoka kwa hiari.
No comments:
Post a Comment