21 September 2013

MSWADA WA KATIBA MPYA:RAIS KIKWETE SASA MTEGONI

  • NI KUTOKANA NA SHINIKIZO ANALOPATA KILA KONA
  • JUKWAA LA KATIBA, CHIKAWE, WAPINZANI WAVAANA 


 Na Darlin Said
Jukwaa la Katiba limemtaka Rais Jakaya Kikwete , asisaini Mswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na badala yake atafute njia mbadala ya kuunusuru ikiwa ni pamoja na kurejeshwa bungeni ili ujadiliwe upya.Kauli hiyo ya Jukwaa la Katiba inaonekana kugeuka mtego kwa Rais Kikwete, kwani imetolewa siku moja baada ya Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe, kumuomba Rais asaini mswada huo ili kuepusha vurugu zitakazoweza kujitokeza katika kikao kijacho cha Bunge kinachotarajia kuanza Oktoba, mwaka huu.

Mbali na Jukwaa la Katiba kutaka Rais Kikwete asisaini mswada huo, vyama vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi, vimezidi kutafuta kuungwa mkono na wadau mbalimbali kwa lengo la kushinikiza mswada huo usisainiwe.Kauli ya kutaka Rais asisaini mswada huo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mchakato wa katiba ulipofikia na matukio yaliyotokea bungeni.
  Kibamba alisema wanashangazwa na kauli ya Waziri Chikawe ya kumshinikiza Rais Kikwete asaini mswada huo wakati yeye (Rais Kikwete) ni kiongozi wa juu serikalini."Inashangaza kusikia Waziri Chikawe akisema kama Rais Kikwete atasaini mswada huo basi ataingia mgogoro na Bunge," alisema Kibamba na kuongeza kuwa hali hiyo ya kumlazimisha asaini au asisaini mswada huo ikiendelea anaweza kuvunja Bunge kwa mujibu wa katiba.
  Kibamba, alisema mchakato wa Katiba Mpya kwa sasa upo njia panda, hivyo njia pekee ya kuunusuru ni Rais Kikwete, kurejesha bungeni ili ujadiliwe upya."Mjadala mkali uliojitokeza bungeni na kusababisha fujo na uvunjifu wa amani ni ishara ya mchakato wa Katiba Mpya kuwa njia panda na kuanza kukosa maelewano, uvumilivu na mwafaka ambayo ni misingi mikuu ya kuongoza mchakato huo,"alisema Kibamba.
Alibainisha kwamba kwa tukio hilo la bungeni, tathmini ya Jukwaa la Katiba inaonesha kuwa masilahi ya vyama vya siasa yametangulizwa badala ya hoja za wananchi. Kibamba, alisema Naibu Spika, Job Ndugai, alikuwa na nafasi ya kuahirisha mjadala mzima wa mswada huo baada ya vyama vya siasa kuususia hadi pale mambo yaliyokuwa yakigombewa yatatuliwe

No comments:

Post a Comment