Na Mwandishi Wetu
TIMU za wavulana na wasichana wenye umri
chini ya miaka 17, ambazo zitaiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya kimataifa
ya Airtel Rising Stars, zinaingia kambini jijini Dar es Salaam kesho kufanya
maandalizi ya mwisho kabla ya kwenda nchini Nigeria kushiriki michuano hiyo.
Akizungumza Dar
es Salaam jana Ofisa Uhusiano wa Airtel Tanzania, Jane Matinde alisema
wachezaji hao chipukizi watashughulikia kukamilisha hati zao za kusafiria kati
ya leo na kesho."Kwa upande wetu kila kitu kimekamilika
kwa ajili ya safari kwenda kwenye mashindano hayo ya kimataifa, ambayo
yatashirikisha timu kutoka sehemu mbalimbali barani Afrika," alisema.
Jane alisema jumla ya wavulana na
wasichana 32 walifuzu kwenda kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano hayo,
baada ya kuonesha uwezo mkubwa wa kucheza mpira wa miguu, wakati wa fainali za
Taifa za Airtel Rising Stars, zilizofanyika Dar es Salaam Juni.Alisema mashindano hayo ya kimataifa
yanafanyika kwa mara ya pili mwaka huu, yakiwa na lengo la kutoa fursa zaidi
kwa wachezaji chipukizi kuendeleza vipaji vyao.
Kwa mara ya kwanza mashindano ya
kimataifa ya Airtel Rising Stars yalifanyika jijini Nairobi mwaka jana, ambapo
Tanzania iliwakilishwa na timu ya wavulana pekee ambayo hata hivyo ilitolewa
hatua za awali, huku timu ya Nigeria ikitawazwa kuwa mabingwa."Kulingana na kiwango cha
kuridhisha cha wachezaji waliochaguliwa mwaka huu, nina imani kwamba timu zetu
za Tanzania wasichana na wavulana zina nafasi nzuri ya kufanya vizuri,"
alisema.
Alisema Airtel imeanzisha mashindano
hayo ya vijana barani Afrika kwa nia ya kusaidia upatikanaji wa vijana wenye
vipaji vya soka kuanzia ngazi ya chini hadi taifa.Ofisa huyo alisema Airtel Rising Stars,
inatoa fursa kwa vijana kudhihirisha uwezo wao kwa makocha wa taifa na
kimataifa na kuweza kujiendeleza zaidi kisoka.
Airtel Rising Stars ni moja ya matukio
ya kisoka ambayo yapo kwenye kalenda ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF). Huanzia katika hatua ya usajili ikifuatiwa na mechi za mtoano, ili
kupata wachezaji nyota wa kuunda timu za mikoa ambazo huchuana katika ngazi ya
taifa
No comments:
Post a Comment