18 September 2013

CHADEMA, CUF, NCCR RUKSA



 Na Mariam Mziwanda
JUKWAA la Katiba nchini, limebariki uamuzi wa vyama vya siasa ambavyo vimeungana, kutumia nguvu ya umma ili iweze kuingilia kati mchakato wa Katiba Mpya usiburuzwe na watu wachache badala yake uzingatie matakwa ya Watanzania.

Vyama hivyo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha NCCR- Mageuzi.Baraka hizo zimetolewa Dar es Salaam jana katika kikao kilichoshirikisha Wenyeviti wa Taifa wa vyama hivyo na Mwenyekiti wa jukwaa hilo, Bw. Deus Kibamba.
Wenyeviti hao ni Bw. Freeman Mbowe (CHADEMA), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na Bw. James Mbatia (NCCR- Mageuzi).Katika kikao hicho, Bw. Kibamba alisema jukwaa hilo linaunga mkono uamuzi huo wa kuwafikia wananchi na kudai kuwa hatua hiyo itaunganisha sauti ya pamoja na kuuondoa mchakato huo katika njia panda kama ilivyo sasa.
"Mchakato huu usihusishwe kisiasa, vyama hivi kuanzia Septemba 21 mwaka huu, vitaanza kufanya ziara za kuwafikia wananchi ili kufikisha kilio cha kupinga Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013.
"Muswada huu unatarajiwa kufikishwa kwa Rais Jakaya Kikwete baada ya kupitishwa bungeni hivi karibuni, jambo la msingi tunapowafikia wananchi, tuzingatie suala zima la amani na utulivu kwani harakati kama hizo huwa na vurugu hivyo ni vyema kutumia busara na uzalendo," alisema.
Bw. Kibamba amevitaka vyama vingine vya siasa, Serikali, viongozi mbalimbali, wadau na wanaharakati kuendelea kushauriana na jukwaa hilo ambalo limetoa fursa ya kupokea maoni na kujadili mchakato wa katiba kabla hawajamuona Rais Kikwete.Alisema wanataka kumuona Rais Kikwete waweze kushauriana kwa lengo la kupatikana katiba iliyo bora kwa wananchi.
Kwa upande wake, kiongozi wa muungano wa vyama hivyo, Prof. Lipumba amesema umoja huo unasononeshwa na kitendo cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuuburuza mchakato huo watakavyo jambo ambalo halipaswi kuvumiliwa.
"Tutaendelea kupiga kelele na kumtaka Rais Kikwete asisaini mswada huu, hatuna mpango wa kwenda kumuona bali tuna mikakati ya kulipua moto kwa wananchi Septemba 21 mwaka huu ili kupata nguvu ya kuzuia mchakato huu.
"Muswada huu umewatenga wananchi wa Zanzibar ambao hawajashirikishwa ipasavyo, pia tunatarajia kukutana na Baraza la Waislamu nchini (BAKWATA), Shura ya Maimamu, Asasi za Watu wenye Ulemavu, madhehebu ya kikristo, vyuo vikuu, wakulima, taasisi na asasi zingine ili kujadili namna ya kupata katiba waitakayo Watanzania.

No comments:

Post a Comment