26 September 2013

MWANAMKE AWATOKEA ‘PUANI’ WATU WATATU

  • MAHAKAMA KUU YAWAHUKUMU KUNYONGWA HADI KUFA


Na Moses Mabula, Nzega
Mahakama Kuu Kanda ya Tabora imewahukumu watu watatu kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kwa makusudi mkazi wa Kijiji cha Mbagwa wilayani Nzega mkoani Tabora,Mganga Mgisha, ili mmoja wa wauaji hao apate fursa ya kuoa mke wa marehemu huyo.

Katika kesi hiyo, mmoja wa wauaji hao, Kulwa Makomelo alikuwa na njama za kutaka kumuoa mke wa marehemu huyo,Catherine John, ambapo ilidaiwa alimlipa kiasi cha sh. 20,000 muuaji mwenzake, Kisena Lutonja, ili amsaidie kufanikisha mauaji hayo.
Mke wa marehemu huyo ni miongoni mwa waliohukumiwa adhabu hiyo. Akitoa hukumu hiyo iliyochukua muda wa saa tatu, Jaji Amiri Mluma, alisema mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa kuwa washtakiwa hao walipanga mauaji hayo.
  Alisema washtakiwa wamepatikana na shtaka hilo la kupanga kuua na kufanya mauaji."Walipanga makusudi kumuua Mugisa, hivyo mahakama inawahukumu kunyongwa hadi kufa ili iwe fundisho kwa watu wengine.
   Jaji huyu aliiambia mahakama hiyo kwamba; "Kutokana na kukithiri kwa vitendo vya watu kushambuliana kwa mapanga bila sababu na kujichukulia sheria mkononi natoa adhabu hii ili iwe fundisho kwa watu wa aina hiyo."
  Awali, mwanasheria wa Serikali, Iddforce Makandara, aliiambia mahakama hiyo kuwa watuhumiwa hao wote kwa pamoja walimuua, Mugisa kwa kumpiga kitu kizito kichwani na kisha kumshambulia kwa mapanga hadi kufa.Aliiambia mahakama hiyo kuwa mwaka 2005 watuhumiwa hao walikula njama za kumuua Mugisa ambaye ni mume wake na Catherine John.
  Alidai kuwa walifanya hivyo ili mjane wa marehemu aolewe na Makomelo, huku Lutonja akilipwa sh. 20,000 ili amsaidie kufanikisha mauaji hayo.Makandara aliomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa washtakiwa hao ili iwe fundisho kwa watu wanaojichukulia sheria mkononi

 

No comments:

Post a Comment