26 September 2013

MAOMBOLEZO

  • RAIS KENYATTA ATANGAZA SIKU TATU ZA KUOMBOLEZA
  •  JESHI LA KENYA LAHITIMISHA KIBARUA KIGUMU
  •  AL SHABAAB WADAI MATEKA 137 WAMEUAWA,WAONYA
 Waandishi  Wetu  n a Mashirika ya Kimataifa
   Kenya imeanza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kwa waathirika wa mashambulizi ya kigaidi yaliyofanyika katika jengo la kibiashara la Westgate mjini Nairobi na kusababisha mapigano yaliyodumu kwa siku nne
. Rais Uhuru Kenyatta amesema bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia jana kwa heshima ya waliopoteza maisha yao katika mashambulizi hayo. Katika hotuba yake kwa taifa juzi usiku, Rais Kenyatta alisema kuwa alihisi uchungu mkubwa na kuwa Kenya imejeruhiwa vibaya, lakini alielezea matumaini kwa kuwa shambulizi limeisha na kusema kwamba waliohusika watakiona cha mtemakuni.

Juzi Rais Kenyatta ametangaza kuwa operesheni za kijeshi dhidi ya magaidi zimemalizika katika maduka ya kifahari ya Westgate.Alisema Kenya imewaaibisha washambuliaji hao, kwa kuua magaidi watano na kuwakamata wengine 11 ambao wamezuiliwa. Katika tukio hilo Watu 62 wameuawa ikiwemo wanajeshi watatu na wengine 8 wamejeruhiwa. Habari kutoka Kenya zinaeleza kuwa kuna hofu kuwa idadi ya watakaofariki huenda ikaongezeka.

Maafisa wa uchunguzi wa kimataifa wanaungana na wale wa Kenya kujaribu kuondoa miili ambayo imenaswa kwenye vifusi vya jengo hilo ambalo sehemu yake iliporomoka jana.Nia ni kujaribu pia kutambua uraia wa washambuliaji hao. Baraza la usalama wa kitaifa lilitarajiwa kukutana jana kudadisi yaliyotokea na kujiandaa kwa mkakati mpya wa kukabiliana na magaidi.

Magaidi watatu wa kundi la Al Shabaab lililokiri kutekeleza mashambulizi hayo,waliuawa katika shambulizi hilo lililodumu kwa siku nne na kuwa washukiwa we n g i n e 11 wa l i k ama twa wakijaribu kuondoka nchini.Wakati huo huo, ofisa mmoja mkuu wa serikali ya Somalia, amesema kuwa hakuna suluhu la kijeshi kwa kundi la wanamgambo wa Al Shabaab nchini humo. Wanamgambo hao wamekiri kuhusika na mashambulizi ya kigaidi nchini Kenya.

  Akizungumza na mjumbe wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa, Yusuf Mohamed Ismail Bari Bari, alisema kuwa serikali yake na jamii ya kimataifa inapaswa, kuangazia zaidi mizizi ya tatizo la magaidi hao, upatikanaji wa rasilimali pamoja na uwakilishi wa kisiasa.Wakati huo huo, Wataalamu wa uchunguzi wa Kisayansi kutoka nchini Ufaransa na Israel wamewasili nchini Kenya kushirikiana na wazawa ili kujua silaha zilizotumika wakati wa shambulizi hilo la kigaidi.

  Wataalam hao wanalenga kubaini ni aina gani ya milipuko ilitumika kulipulia jengo hilo.Pia maofisa wa Serikali bado wapo eneo la tukio ili kuhakikisha usalama unakuwepo. Televisheni ya nchi hiyo ya Q TV imesema kuwa kazi ambayo ilikuwa nimeanza ni ya kuondoa vifusi ili kuweza kuondoa maiti zilizofukiwa baada ya sehemu ya jengo hilo kuanguka.

   Kwa mujibu wa matangazo hayo maiti hizo zitatambuliwa kwa kutumia kipimo cha DNA. Matangazo ya televisheni hiyo yalieleza kuwa ndani ya jengo hilo la kibiashara moshi mkubwa ulikuwa ukizidi kufuka lakini hakukuwa na taarifa zozote kwa waandishi wa habari kuhusu ni nini kilichokuwa kikiendelea.

   Katika hatua nyingine, Serikali ya Kenya imetangaza donge nono la dola milioni 25 kwa mtu yeyote atakayefanikisha kupatikana kwa magaidi sugu ulimwenguni. Tayari FBI imetoa orodha ya magaidi 23 wanaotafutwa.

   Wakati huo huo, wanamgambo wa Al-Shabaab kutoka Somalia jana walidai mateka 137 waliokuwa wakiwashakilia waliuawa katika jumba la kibiashara la Westgate jijini Nairobi.Kwa mujibu wa shirika la habari la Ufaransa, AFP, idadi kamili ya waliokufa imekuwa ngumu kujulikana na inaweza ikawa ni kubwa zaidi kuliko idadi ya walioorodheshwa kukosekana.

   Wapiganaji hao wenye uhusiano na al-Qaeda, katika ujumbe waliouweka kwenye mtandao wa Twitter, walisema "mateka 137 waliokuwa wakishikiliwa na mujahedeen" wamekufa."Wanamgambo hao pia waliwatuhumu wanajeshi wa Kenya kwa kupiga makombora yenye sumu kuhitimisha mapambano ya kuwasaka.


Matukio ya ubabe wa Al-Shabaab


   Haya ni miongoni mwa mashambulizi makubwa ya kigaidi ambayo yamewahi kutekelezwa katika Kanda ya Afrika Mashariki.


Taarifa zinazohusiana na Kenya

  Septemba 21, 2013: Magaidi walitumia guruneti na bunduki kushambulia jengo la kifahari la Westgate mjini Nairobi, Kenya lenye maduka na mikahawa 80 na kuwaua watu 62 huku zaidi ya 175 wakijeruhiwa.Kundi la kigaidi la Al-Shabaab lilikiri kufanya shambulio hilo.

    Oktoba 2011-Machi 2013: Al Shabaab na wapiganaji wake walifanya mashambulizi kadhaa nchini Kenya na kuwaua zaidi ya watu sitini wakilipiza kisasi kile walichosema ni hatua ya Kenya kupeleka majeshi yake nchini huo kupigana dhidi yao.Serikali ya Kenya ilituma vikosi vyake nchini Somalia baada ya al-Shabaab kufanya mashambulizi kadhaa katika maeneo ya mipakani pamoja na kuwateka nyara watalii wa kigeni.

    Julai 11 , mwaka 2010 : Wanamgambo wa Al Shabaab walilipua mabomu katika mji mkuu wa Uganda Kampala, katika mkahawa ambako mashabiki wa soka walikuwa wanatazama fainali ya michuano ya Kombe la Dunia, kwenye televisheni kubwa.

    Takriban watu 76 waliuawa. Kundi la Al-Shabaab lilisema kuwa mashambulizi hayo yalikuwa ya kulipiza kisasi kwa Uganda kujihusisha na vita dhidi ya kundi hilo Somalia.Novemba 28, mwaka 2002: Kundi hilo la kigaidi lilishambulia hoteli ya kifahari iliyokuwa inamilikiwa na Waisraeli, katika eneo la Kikambala karibu na mji wa Mombasa na kuwaua watu 13.

   Dakika chache kabla ya shambulizi hilo, magaidi hao waliifyatulia makombora ndege ya Israel iliyokuwa inaruka katika Uwanja wa Kimataifa wa Mombasa, lakini waliikosa.Agosti 7, mwaka 1998: Kundi lingine la kigaidi la al-Qaeda lilishambulia balozi za Marekani mjini Nairobi na Dar es Salaam. Mashambulizi hayo yaliwaua watu 224 , wengi wakiwa Wakenya . Raia 123 wa Marekani pia waliuawa.





























No comments:

Post a Comment