Na Amina Athumani
KATIBU Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako
amesema ataondoka katika klabu hiyo, endapo uongozi wake utamtaka afanye hivyo.Mwalusako
ambaye alikaimu nafasi ya Katibu Mkuu kwa muda mrefu sasa, alisema yupo tayari
kukabidhi ofisi za klabu hiyo na kuiachia nafasi aliyokuwa akikaimu.
Akizungumza Dar
es Salaam jana, Mwalusako alisema ataondoka katika klabu hiyo iwapo uongozi wa
klabu hiyo utamtaka kufanya hivyo mara baada ya ujio wa Katibu Mkuu mpya wa
klabu hiyo Patrick Naggi.
Alisema kwa
sasa bado anaendelea kufanya kazi na kushikilia wadhifa alionao kwa kuwa hakuna
kiongozi yeyote aliyeongea naye kuhusu ujio wa katibu mpya.
Alisema licha
ya katibu huyo kwenda makao makuu ya klabu hiyo kujitambulisha kuwa ameajiriwa
kama Katibu Mkuu hakuna kiongozi yoyote aliyeongea naye wala kumpa maelezo ya
aina yoyote.Alisema yeye bado yupo ofisini na
hajatambulishwa mtu yoyote hadi jana ,ila kama watakuja na kumleta na
kumtambulisha yeye atakabidhi ofisi na kuendelea na shughuli zake nyingine.
Kwa upande wa wanachama wa klabu hiyo,
walisema hawatambui ujio wa katibu huyo na hakuna kiongozi yoyote mwenye
mamlaka ya kuajiri bila kuwashirikisha wanachama.Wakizungumza katika makao makuu ya
klabu hiyo jana, wanachama hao walisema ujio wa Katibu huyo ni mwanzo wa
kuvurugika kwa klabu hiyo ikiwa ni pamoja na kuendeshwa kwa kufuata mwongozo wa
mtu mmoja.
Kauli ya Mwalusako na wanachama hao
imekuja siku moja baada ya Baraza la Wazee la klabu hiyo kutoa tamko la
kumpinga katibu huyo kufanya kazi za klabu hiyo.Katibu wa Baraza la Wazee la klabu
hiyo, Ibrahim Akilimali, alisema wanamtambua Mwalusako kuwa ndiye mtendaji wa
klabu hiyo na si Naggi.
Akilimali alisema kwa mujibu wa katiba
ya Yanga endapo kunahitajika mabadiliko ya kiutendaji kunaitishwa kikao cha
Kamati ya Utendaji kujadili suala hilo, jambo ambalo halikufanyika.
Naggi aliripoti juzi katika klabu hiyo na kujitambulisha kuwa Katibu
Mkuu mpya wa klabu hiyo kwa kuchukua nafasi ya Mwalusako aliyekuwa akikaimu,
ambapo katibu huyo aligonga mwamba baada ya wanachama kukataa na kudai
kutomtambua.
No comments:
Post a Comment