Na
Elizabeth Joseph, Dodoma
Mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina
la Cecilia Laurent (28) mkazi wa Uhindini mkoani Dodoma ambaye ni mhudumu wa
baa na nyumba ya kulala wageni ijulikanayo kama CDA Club mkoani hapa
anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumuua mtoto wake mchanga.
Akielezea tukio hilo jana Muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Mary Motto alisema kuwa mwanamke huyo alipokelewa majira ya saa 8 usiku ambapo pia hakuwa na kadi ya kliniki jambo ambalo lilidhihirisha kuwa hajahudhuria kliniki tangu kushika ujauzito huo, lakini walimpokea.
“Cecilia alifika hapa saa 8 usiku, bila ya kadi ya kliniki na ilipofika majira ya saa 9 usiku alienda chooni na kujifungua mtoto wa kiume, bila kutoa taarifa kwa wauguzi na baada ya kujifungua akamsukumiza mtoto katika tundu la choo kisha akafungua bomba la maji ili kukisukuma kiumbe (kuflash) jambo ambalo lilishindikana kutokana na tundu la choo hicho kuwa dogo kupitisha kiumbe hicho," alidai Muuguzi huyo.
Mmoja kati ya mashuhuda waliokuwa wodini hapo aliyejitambulisha kwa jina la Nyamizi Muhosi alisema kuwa, wakati akiwa bafuni anafua alimuona mwanamke huyo akianza kuzaa akiwa kachuchumaa kwenye tundu la choo, ndipo alipomkataza na kumwambia awaite wauguzi jambo ambalo hakulisikiliza.
“Nilikuwa bafuni nafua. huyo Cecilia alikuja chooni nikaona mtoto kashaanza kutoka nikamwambia awaite wauguzi wa zamu, lakini alikataa na kuendelea kuzaa mwenyewe bila kusaidiwa kisha akakisukumiza kichwa cha mtoto wake katika tundu la choo na kufungulia maji (kuflash) ili kuzidi kumsukuma, halafu akaanza kupiga kelele akidai mtoto wake kadumbukia chooni kwa bahati mbaya, jambo ambalo si la kweli,”alisema Muhosi.
Shuhuda mwingine
aliyejitambulisha kwa jina la Mary Chihuma alidai kuwa, mwanamke huyo
alidhamiria kuua mtoto wake, kwani tangu alipofika wodini hapo alikuwa
akijigonga kwa makusudi katika vitanda vya wagonjwa wengine, lakini
walipomuhoji kwa nini anafanya hivyo hakuwajibu kitu.Mtu mwingine aliyejitambulisha kwa jina
la Juma Alikanda alikemea kitendo hicho na kusema kuwa si cha kiungwana na kama
hali ya maisha yake ni ngumu haikumpasa kuchukua maamuzi hayo na kuitaka
serikali kuchukua hatua za kisheria ili kukomesha tatizo hilo.
Kwa mujibu wa mfanyakazi mwezake na
mtuhumiwa huyo ambaye hakutaka jina lake
litajwe alisema kuwa,
mtuhumiwa huyo alikuwa akiongopa kuhusu miezi ya mimba yake kwa kutaja miezi
tofauti tofauti ambapo hata shangazi yake alikuja hivi karibuni kwa ajili ya
kumuangalia, lakini mtuhumiwa huyo alimjibu mimba ni ya miezi minne jambo
lililomfanya shangazi huyo kurudi kijijini kwao Usandawe Kondoa mkoani hapa.
Akithibitisha
kutokea kwa tukio hilo kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa
Upelelezi mkoani humo, ASP Damas Nyanda alikiri kutokea kwa tukio hilo na
kuongeza kuwa mwili wa kichanga hicho umehifadhiwa katika chumba cha maiti
katika Hospitali ya Rufaa mkoani hapa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
No comments:
Post a Comment