26 September 2013

MANJI AWATULIZA WACHEZAJI YANGA Na Mwandishi Wetu
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji amewatuliza wachezaji wa timu hiyo na kuwataka wakaze buti katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom zinazokuja

Manji aliwatuliza wachezaji hao juzi alipokutana nao katika hoteli ya Serena, Dar es Salaam kwa ajili ya kula chakula cha usiku pamoja na viongozi wengine wa Yanga.Katika mechi za ligi hiyo, ambazo Jumamosi itafikia mzunguko wake wa sita, Yanga ina pointi sita ikiwa imeachwa na watani wao wa jadi Simba yenye pointi 11 kileleni.
Manji aliwataka wachezaji hao, wasimlaumu mtu kwa matokeo waliyoyapata na badala yake kuelekeza nguvu katika mechi zilizobaki.Akizungumzia suala la baadhi ya wachezaji kudai fedha za usajili, Manji alisema tatizo hilo litashughulikiwa haraka iwezekanavyo ili kila mmoja apate chake.
  Katika hatua nyingine, mchezaji aliyesajiliwa kutoka Simba Mrisho Ngassa ametakiwa kulipa deni la faini sh.milioni 45 kwa Simba kwa kosa la kusaini katika timu mbili. Habari kutoka ndani ya Yanga, zimeeleza kuwa mchezaji huyo anatakiwa kulipa fedha hizo kwa kuwa tayari walishamalizana na kama klabu ikilipa atalazimika kuongeza mkataba wa kuichezea timu hiyo miaka mitatu.
  Chanzo hicho kimeeleza kwamba Yanga inamtaka Ngassa, kulipa fedha hizo kwa kuwa hazikuisaidia klabu bali zilimfaidisha yeye binafsi.
Ngassa alipotafutwa jana kuzungumzia suala hilo simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila kupokelewa.

No comments:

Post a Comment