06 September 2013

MAGUFULI: WAHANDISI WAAPISHWE



Anneth Kagenda na Theophan Ng'itu
SERIKALI imeitaka Bodi ya Usajili ya wahandisi (ERB), ihakikishe inawaapisha Wahandisi 12,500 na viongozi wa Idara za Taaluma hiyo ndani ya mwaka mmoja.Mhandisi ambaye atagoma kuapishwa, atangazwe kuwa ni mlarushwa pamoja na kufutiwa leseni yake.Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli, alitoa agizo hilo Dar es Salaam jana katika maadhimisho ya Siku ya Wahandisi na kuwataka wazingatie hilo ili waendelea kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa
.Alisema ni wakati mwafaka kwa wahandisi nchini, kufanya mabadiliko ya utendaji kazi na kutoa upinzani kwa wageni kwani wakifanya hivyo, watakuwa wamejiweka katika nafasi mzuri."Serikali kupitia Wizara yangu, inatambua thamani mliyonayo hivyo naomba mfanye kazi zenu kwa uadilifu mahali popote iwe serikalini, katika sekta binafsi na sehemu nyingine.
"Ulaji wa kiapo hiki, utasaidia pale Mhandisi anapokwenda kinyume na sheria, utaratibu uliowekwa, bodi itaweza kumwajibisha," alisema.Alisema Uhandisi ni taaluma iliyobeba jukumu la kuleta maendeleo ya nchi husika ambapo kila idara inahitaji wahandisi hivyo umefika wakati wa kubadilika na kutoa upinzani kwa wageni.
Alisema Serikali haitaki kukusanya mapato yake kwa shida wakati asilimia kubwa fedha hiyo, inachukuliwa na watu kutoka nje ya nchi jambo ambalo si busara.Dkt. Magufuli kwa kushirikiana na Mwanasheria wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Warialwande Lema, aliwaapisha Wahandisi 50 waliokula kiapo cha utii wa taaluma yao.
Aliwataka kufanyia kazi viapo hivyo ambavyo vitawaumbua wahandisi wasio makini na taaluma yao. Aliitaka ERB kuhakikisha fedha za miradi inayotolewa kwa wahandisi mbalimbali ndani na nje ya nchi, zinabaki nchini kwa kile alichosema lazima heshima ya nchi irudi na hadhi kwa taaluma ya Uhandisi.
Alisema hivi sasa, Serikali imeanzisha mpango wa "Big Result Now" (Matokeo Makubwa Sasa), ambao kipaumbele chake ni miundombinu ambayo itawategemea wao hivyo Serikali haitapenda kuona mabilioni yaliyotengwa kwa mpango huo yakienda nje.
"Serikali inaendelea kuandaa mazingira bora kwa wahandisi pamoja na kuwapendelea katika miradi, kutenga fedha za ujenzi wa vyuo, kusomesha wanafunzi nje ya nchi na kutoa tuzo za kushawishi watu kujiunga na taaluma hii...hadi sasa zimetengwa sh. milioni 500 kwa ajili ya kuwapeleka wanafunzi 2,500 nchini Norway," alisema.Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mhandisi Ninatubu Lema, alisema Mhandisi anapokiuka masharti ya leseni, bodi haina budi kumchukulia hatua za kisheria.

No comments:

Post a Comment