06 September 2013

ALIYENG'ATWA USONI AOMBA MSAADA



 Na Mwandishi Wetu
MKAZI wa Kijiji cha Nyabibuye, Wilaya ya Kibondo, mkoani Kigoma, Kasusula Imani (16), aliyejeruhiwa vibaya usoni na bosi wake Imani Paulo (36), amewaomba Watanzania wamsaidie kwa hali na mali ili aweze kwenda kutibiwa nje ya nchi.Akizungumza na Majira jana kwa njia ya simu akiwa katika Hospitali ya Bugando, mkoani Mwanza ambako amelazwa, Bw. Imani alisema kutokana na tukio hilo, kwa sasa hawezi kuona.

“Bosi wangu alinijeruhi kwa kuninyofoa macho, pua, mdomo na vipande kuvimeza...sasa nimelazwa hapa Bugando, nahitaji msaada zaidi wa kwenda kutibiwa nje ya nchi,” alisema.Alisema amelazwa hospitalini hapo zaidi ya miezi miwili lakini bado hali yake haijaweza kurejea kama awali.
“Mimi sijapona...kama baba yangu angekuwa hai labda angenisaidia kupata matibabu zaidi kwani mama yangu hana uwezo kiasi kwamba hata nauli ya kufika hospitali kutoka Kigoma hadi Mwanza hana na mimi nakaa peke yangu,” alisema.
Aliongeza kuwa, yeye ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto watano na alishindwa kuendelea na masomo baada ya baba yake kufariki akiwa darasa la pili hivyo aliamua kufanya kazi aweze kushirikiana na mama yake kuwalea wadogo zake.
Imani alisema baada ya kupatwa na tukio hilo, hivi sasa anaishi kwa shida ambapo Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Bw. Venance Mwamotto, alisema kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa huo, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, wanafanya jitihada za kuhakikisha anakwenda kutibiwa nchini India.
“Tupo katika harakati za kuhakikisha anakwenda kutibiwa India, kwa sasa tupo katika maandalizi ya kumfungulia akaunti,” alisema.
Aliwaomba Watanzania kumsaidia fedha kijana huyo aweze kwenda kutibiwa nchini India na mtu yeyote mwenye mchago awasiliane na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Kibondo au auwasilishe katika ofisi za Majira, zilizopo Gerezani, Kariakoo, Mtaa wa Lugoda.
Kijana huyo aliyeruhiwa na bosi wake ambapo kabla ya kumjeruhi, anadaiwa kumkaba koo mbwa wake, kula ulimi wake na kufariki dunia ndipo alimrukia Imani, kumnyofoa pua na macho.Mtuhumiwa huyo alikamatwa, kufikishwa Kituo cha Polisi Kibondo kisha kufikishwa mahakamani. Hata hivyo, mshtakiwa huyo akiwa rumande katika Gereza la Nyamisivi, alimng’ata, kula kipande cha nyama ya mguu mshtakiwa mwenzake hivyo uongozi wa gereza ulilazimika kumtenga na wenzake.

No comments:

Post a Comment