Na Mwandishi Wetu, Simiyu
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana,
amewataka wabunge wa chama hicho kuwahimiza mawaziri ili waweze kutimiza wajibu
wao wa kutumikia wananchi tofauti na ilivyo sasa ambapo wengi wao wanafanya
kazi kwa mazoea
. Kinana alisema kasi ya kufuatilia utendaji kazi wa mawaziri
inayofanywa na Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina ni ya kuridhisha na kwamba
chama hicho kinaheshimu msimamo wa mbunge huyo katika kuisimamia kikamilifu
Serikali ili iweze kutimiza malengo ya kuwaletea maisha bora Watanzania.
Alisema Mpina ni mbunge hodari na jasiri aliyemstari wa mbele
kuwatetea wananchi na kuhoji uwajibikaji wa Serikali awapo bungeni, hivyo chama
hicho kitaendelea kuthamini mchango wake kwani kwa kiasi kikubwa unasaidia
kuharakisha utendaji wa Serikali.
"Mbunge wenu ni hodari, sisi chama tunamheshimu, ni
mchapakazi, mtetezi wenu na tunaamini mtaendelea kumchagua katika Uchaguzi Mkuu
ujao,"alisema Kinana. Alisema matatizo mengi ya wananchi yanashindwa kutatuliwa kutokana
na Mawaziri kukaa maofisini bila kufika katika maeneo husika na kwamba
ufuatiliaji wa Mbunge huyo kwa kiasi kikubwa utasaidia kuwaamsha ili waweze
kuchapa kazi inayotegemewa na wananchi.
Pia alisifu uwajibikaji wa Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Rosemary
Kirigini katika kufuatilia kero za wananchi na kuwataka viongozi wengine kuacha
kusubiri hadi madhara yatokee ndipo wakimbilie kwenye maeneo hayo kutafuta
suluhu.
Kwa upande wake Mpina alisema mapokezi makubwa aliyopata Katibu
Mkuu huyo wa CCM ni ishara tosha kuwa Serikali imekuwa ikiwajibika kwa wananchi
hasa katika jimbo hilo kwa kufanikisha kutelekezwa kwa ahadi za Rais Jakaya
Kikwete alizotoa kwenye kampeni ikiwa ni pamoja na ujenzi wa daraja la
Mongo-obakima ambapo wananchi walipoteza maisha kwa kuliwa na mamba na viboko
pamoja na kusombwa na maji.
Katika mkutano huo wananchi hao walimuomba Katibu Mkuu huyo wa CCM
kuwatafutia suluhu ya tatizo la malisho ya mifugo hususan kwa wananchi
wanaoishi kando ya pori la akiba la Maswa kutokana na baadhi ya viongozi
kuwabambikia kesi na kuwakamua fedha zao kupitia mgogoro huo wa malisho ya
mifugo.
Kufuatia ombi hilo Kinana aliwaagiza Mawaziri wa Maliasili
na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Profesa Anna Tibaijuka kufika katika eneo hilo na kuutafutia ufumbuzi
mgogoro huo.
No comments:
Post a Comment