05 September 2013

KESI DHIDI YA PINDA YAIVA

Na Rehema Mohamed
KESI ya kikatika iliyofunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) dhidi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, inatarajiwa kuanza kuunguruma Septemba 16, mwaka huu katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana mahakamani hapo, Dar es Salaam jana kesi hiyo italetwa kwa ajili ya kutajwa kwa mara ya kwanza tangu ifunguliwe.Shauri hilo litatajwa mbele ya jopo la Majaji watatu watakaosikiliza shauri hilo ambao ni Jaji Kiongozi Fakhi Jundu, Augustine Mwarija na Dkt. Fauz Twaib.
LHRC na TLS walimfungulia Waziri Mkuu kesi hiyo kutokana na kauli yake aliyoitoa bungeni ya kuruhusu vyombo vya usalama kuwapiga watu wanaokataa kutii sheria zinazotolewa na vyombo hivyo.Mbali na Pinda mwingine aliyeunganishwa katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambapo kwa upande wa LHRC inawakilishwa na mawakili zaidi ya 20.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Waziri Pinda, anakabiliwa na tuhuma za kudaiwa kuvunja katiba ya nchi kwa kuruhusu askari kuwapiga wananchi.Mkurugenzi wa LHRC, Dkt. Hellen Kijo Bisimba wakati akifungua mashtaka hayo katika Mahakama Kuu alisema kuwa wanamshtaki Waziri Mkuu kwa maelezo kuwa amekiuka kifungu cha Katiba Ibara 13 (1).
Pinda ametajwa kuwa ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo namba 24.Naye Mjumbe wa Bodi ya LHRC, Wakili Dkt. Ringo Tenga, alisema katika kesi hiyo wameangalia zaidi sheria na hasa haki za msingi za binadamu na kwamba kauli hiyo ya Waziri Mkuu Pinda inahatarisha haki hizo.
Hata hivyo hatua hiyo ya LHRC ilipingwa vikali na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), Dkt. Elieza Feleshi, akisema hakuna uhalali wa mashtaka yoyote dhidi ya kiongozi huyo sababu kauli ya Pinda kuwa pigeni haikuwa ya piga ua.

No comments:

Post a Comment