Na Mwandishi Wetu, Gambia
KOCHA Mkuu wa timu ya taifa (Taifa
Stars), Kim Poulsen amesema kukosekana kwa wachezaji tisa muhimu ni mojawapo ya
sababu za kushindwa mechi ya Jumamosi na akaiomba TFF kuhakikisha kuwa
wachezaji wanaocheza nje wakiitwa wanakuja nyumbani kucheza.
Poulsen
aliyasema hayo mjini Banjul nchini hapa, mara
baada ya mchezo na Gambia
ambapo wenyeji walishinda kwa mabao 2-0 katika mechi ya mwisho ya kuwania
kucheza fainali za Kombe la Dunia.Alisema alikosa wachezaji tisa muhimu,
ambapo wengine hawakufika kabisa kutoka wanakocheza soka la kulipwa na wengine
walikuwa majeruhi."Nimeambiwa Gambia waliita
wachezaji 11 kutoka nje kwa sababu walitambua umuhimu wa kushinda mechi hii na
sisi tulikosa karibu timu nzima," alisema.
Alisema ni bora TFF wahakikishe
wachezaji hao wanapohitajika hasa kwenye mechi za kufuzu kucheza Kombe la
Afrika, wanapatikana kwa wakati."Tumeijenga hii timu tukiwa na
malengo ya kufuzu kucheza fainali hizo za Kombe la Afrika kwa hivyo ni muhimu
mno wawepo wanapoitwa," alisema Poulsen.
Wachezaji wazoefu wa Stars waliokosa
mechi hiyo ni, Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, Kelvin Yondani, Athuman Idd,
Salum Abubakar, John Boko, Mwinyi Kazimoto, Shomari Kapombe na Aggrey Morris.Alisema baadhi yao
ambao ni vijana, wamejipatia uzoefu mkubwa pamoja na kwamba walifanya makosa
kadhaa uwanjani, ambayo anaamini kama
wachezaji wenye uzoefu wangekuwepo wangeweza kudhibiti ile hali kwa namna moja
au nyingine.
Hata hivyo, alisema licha ya timu yake
kushindwa na Gambia, hajakata tamaa kwani malengo aliyojiwekea tangu mwanzo ni
kufuzu kucheza fainali za Kombe la Afrika 2015, jambo ambalo hata TFF na
mdhamini,Kilimanjaro Premium Lager wanalitambua na wanaunga mkono.
Kocha huyo alisema inasikitisha
kupoteza mechi, lakini Watanzania lazima waelewe kuwa malengo ni ya muda mrefu
na timu inaendelea kuimarika siku hadi siku.Alisema huu si muda wa kulaumu na
kukata tamaa, kwani safari bado ndefu na tayari kuna dalili nzuri zinaonekana
hasa tangu, Taifa Stars ipate udhamini mpya wa Kilimanjaro Premium Lager, ambao
unawezesha mambo mengi kufanyika sasa kwani imewekeza zaidi ya sh. bilioni 15
kwa miaka mitano.
"Mechi hizi za Kombe la Dunia
zimetupa uzoefu kwani tumeweza kucheza na timu kubwa kama Ivory Coast na Morocco na kuonesha uwezo mkubwa
zaidi na hii inaonesha kuwa timu imeimarika kabisa," alisema.Kabla ya mechi hiyo, baadhi wa wananchi
wa Gambia walionesha
kutokuwa na imani na timu yao
baada ya kutofanya vizuri katika mechi zilizopita.
Geoffrey Kaishozi ambaye ni Mtanzania
anayefanya kazi Gambia,
alisema alifurahishwa na jinsi Stars ilivyocheza katika kipindi cha kwanza,
lakini cha pili mchezo ulibadilika baada ya Gambia kupata bao dakika ya 45 na
lingine katika kipndi cha pili."Tumesikitika kuwakosa wachezaji
wengi tuliowazoea na pengine kuwepo kwao kungeleta utofauti katika mechi
hii," alisema na kuongeza kuwa ni vema wachezaji wale muhimu wawepo katika
mechi kama hizi.
Naye Francis Mushi alisema alikwenda
uwanjani na matumaini kuwa Taifa Stars, ingeshinda hasa baada ya kuifunga Gambia mabao
2-1 katika mechi ya awali nyumbani."Tulicheza vizuri kipindi cha
kwanza, lakini cha pili tulilemewa na tukaamka dakika za mwisho za mpira;
lakini hatukufanikiwa kupata bao," alisema.
Alisema Gambia pia hawakucheza katika
kiwango chao cha kawaida kwa hivyo wengi walitegemea Taifa Stars ingeshinda.Kwa upande wake, Emmanuel Mtaki ambaye
pia anafanya kazi Gambia,
alisema kulikuwa na makosa mbalimbali kama
mabeki kutowadhibiti vizuri wapinzani wao.
Mabao yote ya Gambia katika
mchezo huo wa Jumamosi, yalifungwa na nahodha wa timu hiyo, Mustafa Jarjue
ambaye alicheza mpira wa hali ya juu.Stars inatarajiwa
kuwasili nchini leo saa 8 mchana kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya.
No comments:
Post a Comment