30 September 2013

BENKI DAR ZAPEWA MASHARTI



Na Rose Itono
  Jeshu la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salam, limesema kuanzia leo benki zote zilizopo jijini humo zitalindwa na askari wa jeshi hilo ili kuzuia wimbi la matukio ya ujambazi katika benki.Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari
. Alisema mtandao huo, unahusisha baadhi ya watumishi wa benki hizo ambao si waaminifu ambapo wahalifu hutumia sare za jeshi hilo kufanikisha uhalifu wao.Aliongeza kuwa, hatua hiyo imelenga kutimiza wajibu wa jeshi hilo kuhakikisha matukio ya aina hii hayatajirudia na kuongeza kuwa, wasiokubaliana na hatua hiyo wafunge benki zao.
  Kamishna Kova alisema, jeshi hilo limebaini ujambazi huo unafanyika kupitia mtandao wa wafanyakazi wa benki ambao wanashirikiana na baadhi ya walinzi wa kampuni binafsi."Matukio haya yanaonesha wahalifu wanakuwa na taarifa muhimu za benki husika pamoja na kujua watunzaji funguo za chumba cha kuhifadhia fedha na kiasi ambacho kimeingia benki.
  "Kutokana na mazingira hayo, jeshi letu likiwa na wajibu wa kulinda maisha ya watu na mali zao, tumechukua hatua madhubuti na makusudi ili kukomesha wizi huo ambao unaendelea," alisema.
   Alisema benki zote jijini humo zitalazimika kufuata utaratibu uliowekwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ili kuhakikisha siri za benki hazivuji kwa wahalifu kama ilivyo sasa.  
   Aliongeza kuwa, matukio kama hayo ni tishio kwa wawekezaji nchini na kuwataka wamiliki wa banki, kutumia vifaa vya kisasa ili kuimarisha ulinzi ambavyo vitatunza kumbukumbu au kutoa tahadhari ya haraka kama kuna tishio la kiusalama.
  Pia alizitaka benki hizo kuwa waangalifu na ajira za wafanyakazi wao kabla ya kuwaajiri na kuwafanyia upekuzi wa kina ambapo jeshi hilo litatoa ushirikiano wa kuweka kumbukumbu za watumishi wao na kuwataka kuwatumia kampuni binafsi za ulinzi zenye viwango vya kulinda na kusafirisha fedha zao.
  Aliwataka wafanyakazi wa benki, kuvaa sare, kupewa mafunzo ya kujihami kiusalama pamoja na mbinu mbalimbali za kuwatambua wahalifu wanaojihusisha na wizi wa mtandao."Tunasisitiza matumizi ya teknolojia ya kisasa kama kamera za CCTV, mawsiliano ya moja kwa moja na vyombo vya dola kabla, wakati au baada ya tukio.
  "Makamanda wote wanapaswa kujipanga upya dhidi ya matukio kama haya, majambazi wanaofanya matukio ya uhalifu, acheni mara moja kwani oparesheni ya kuwasaka na kuwakamata itafanyika katika mikoa yote chini," alisema.
  Kamishna Kova alisema, jeshi hilo linamshikilia mmoja kati ya watu wanaojihusisha na matukio ya aina hiyo, Azim Chokera (47) mwenye asili ya Kiasia ambaye ushahidi wa awali unaonesha amejihusisha na matukio mawili ya wizi wa benki na amekiri kufahamu mwenendo wa tukio la wizi wa Benki ya Habib.

No comments:

Post a Comment