Watu 12
wamefariki dunia katika ajali mbili tofauti ambazo zimetokea mikoa ya Mbeya,
Dodoma usiku wa kuamkia jana.
Katika ajali ya
kwanza, watu sita wamefariki dunia mkoani Mbeya na wengine saba kujeruhiwa
vibaya baada ya gari walilopanda aina ya Toyota Hiace yenye namba T 223
AGQ kuacha njia, kupinduka na kutumbukia mtoni, anaripoti Esther Macha,
Mbeya na Elizabeth Joseph, Dodoma.
Akizungumza na
waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Kamishna Msaidizi wa
Polisi, Diwani Athuman, alisema ajali hiyo imetokea Septemba 22 mwaka huu, saa
mbili usiku, Barabara ya Sokomatola/Stendi Kuu, jijini humo.
Alisema gari
hilo lilikuwa likiendeshwa na dereva aliyemtaka kwa jina la Dunia Francis (38),
mkazi wa Air Port, jijini humo ambaye ni miongoni mwa majeruhi.
“Waliofariki ni
wanawake wawili na wanaume wanne ambao wote hawajafahamika majina yao wala
anuani zao...majeruhi ni Juma Warioba (32) mkazi wa Sae na Mwandela Mwamsi
(22), mkazi wa Majengo.
“Wengine ni
Kambi Ally (32), mkazi wa Iringa, Seleman Shelukindo (25), mkazi wa Ileje, Nuru
Shelukindo (32), mkazi wa Ileje na Bahati Ally (14) mkazi wa Songea ambapo wote
wamelazwa Hospitali ya Rufaa hapa Mbeya,” alisema.
Kamanda Athumani
alisema, breki za gari hilo zilikataa hivyo kupoteza mwelekeo, kupinduka na
kutumbukia katika mto uliopo jirani na Stendi Kuu.
“Bado
tunaendelea kuchunguza chanzo cha ajali, miili ya marehemu imehifadhiwa katika
Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa ajili ya utambuzi, dereva anahojiwa,” alisema.
Wakati huo huo, watu sita
wamefariki dunia papo hapo na wengine 17 kujeruhiwa baada Basi la Kampuni ya
Alsaedy, lenye namba T 433 BLR, walilokuwa wamepanda, kugongana na lori namba T
1O2 CGR, eneo la Chinagali 2 Wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma.
Akizungumzia
ajali hiyo, Mratibu Mwandamizi wa Polisi, Damas Nyanda, alisema ilitokea
Septemba 22 mwezi huu, saa 3:30 usiku, Barabara Kuu ya Dodoma- Morogoro.
Basi hilo
lilikuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Dodoma na lori lilikuwa likitoka Dodoma
kwenda Dar es Salaam.
Waliokufa katika
ajali hiyo ni Nizar Khan (45 ), ambaye ni dereva wa basi, mkazi wa Dar es
Salaam, Hassan Kizigo (30-35), ambaye ni dereva wa lori, mkazi wa Temeke, Dar
es Salaam.
Wengine ni Ahmad
Mohamed (35-40), ambaye ni mmiliki wa lori, mkazi wa Kinyerezi, Dar es Salaam,
Hussein Mashauri(35-40) mkazi wa Kinyerezi, Imran Sharif (20-25) ambaye ni
utingo wa lori, mkazi wa Jijini Dar es Salaam na abiria mmoja wa basi mwanaume
(30-35) ambaye jina lake halijafahamika.
Aliongeza kuwa,
chanzo cha ajali ni mwendo kasi wa dereva wa basi ambaye alishindwa kulimudu na
kusababisha magari hayo kugongana uso kwa uso.
“Kati ya
majeruhi 17, wanaume 10 na wanawake saba, wote wamelazwa katika Hospitali ya
Rufaa Dodoma, miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti
hospitalini hapo ikisubiri utambuzi zaidi,” alisema
No comments:
Post a Comment