Na Mwandishi Wetu, Njombe
NAIBU Waziri wa Kazi na Ajira, Dkt. Makongoro Mahanga,
amesema Serikali haitaivumilia sekta binafsi yoyote ambayo itawalipa
wafanyakazi wake kiwango cha mishahara pungufu ya kile cha kima cha chini
kilichotangazwa na Serikali.
Dkt. Mahanga alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti hivi karibuni
alipokutana na wafanyakazi na viongozi wa Kiwanda cha Maziwa cha CEFA kilichopo
Njombe pamoja na wale wa mashamba ya Chai Lupombe.
Alisema kiwango cha chini kilichotangazwa na serikali ni kiwango
elekezi kinachopaswa kufuatwa na sekta zote na kwamba waajiri wanaweza kulipa
zaidi ya viwango hivyo.
Aliongeza kuwa, wizara yake imekuwa ikipokea malalamiko k u t o k
a kwa b a a d h i y a wafanyakazi kupitia vyama vyao kwa upande mmoja; na
waajiri kwa upande mwingine, kuhusu viwango vilivyotangazwa na serikali kupitia
Waziri wa Kazi na Ajira kwenye baadhi ya sekta.
Alifafanua kwamba viwango hivyo vilitangazwa na Waziri baada ya
kupata ushauri kutoka kwa Baraza la Ushauri la Kazi na Huduma za Kiuchumi na
Kijamii (LESCO) ambalo nalo lilipitia taarifa ya utafiti na mapendekezo ya
kitaalamu.
Dkt. Mahanga alisema badala ya vyama hivyo kukimbilia kwa Waziri,
wangekaa na waajiri wa kampuni mmoja mmoja na kujadili tija na uzalishaji
kwenye makampuni hayo.
"Kama kitaalamu itaonekana viwanda hivyo vina uwezo wa kulipa
viwango zaidi ya vile vilivyotangazwa, basi waajiri na wafanyakazi wakubaliane,
kupitia Mikataba ya Hiari (CBA), kulipa mishahara hiyo ya juu; na Serikali
itatambua mikataba na makubaliano kama hayo," alisema Dkt. Mahanga.
Mwezi wa sita mwaka huu, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia
Kabaka, alitangaza viwango vya kima cha chini cha mishahara kwenye sekta
mbalimbali. Katika tangazo hilo kima cha chini kinaanzia sh. 80,000 kwa mwezi
kwa wafanyakazi wa majumbani, sh. 100,000 kwa sekta za kilimo, viwanda na
ulinzi; na kuendelea kwenye sekta mbalimbali hadi sh 400,000 kwa mwezi kwa
sekta za nishati, utafiti na uchimbaji wa madini na sekta ya fedha.
Hata hivyo, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wafanyakazi
kwa baadhi ya sekta kama viwanda wakidai viwango walivyopangiwa vya sh 100,000
ni vya chini mno.
No comments:
Post a Comment