Penina Malundo na Leah Daudi
BAADHI ya viongozi wa vyama vya siasa
wamemtaka msajili mpya wa vyama vya siasa nchini, jaji Francis Mutungi
atekeleze majukumu yake bila upendeleo kwa chama chochote.Akizungumza na
gazeti hili kwa njia ya simu jana, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi
(CUF) Tanzania Bara, Julius Mtatiro alisema kuwa msajili mpya anatakiwa kufanya
kazi yake kwa umakini bila kupendelea chama kimoja.
Mtatiro
alisema, Msajili huyo akionesha hali ya upendeleo kwa chama kimoja hawatasita
kumweleza ukweli.Alisema kuwa,
Msajili aliyepita (John Tendwa) alionesha wazi kupendelea chama kimoja ambapo
vyama vingine viliondoa uaminifu katika ufanyaji kazi wake.
“Msajili huyu
ni mpya, anatakiwa atekeleze majukumu yake vizuri na kutoonesha hali yoyote ya
upendeleo, kwa baadhi ya vyama na endapo ataonesha hali hiyo hatutaogopa
kumueleza waziwazi kwa kitendo atakachokifanya,” alisema Mtatiro.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR
Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema kuwa msajili mpya anatakiwa kusimamia vyama
vya siasa kwa ukaribu na kujua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika
vyama.
Pia alisema, changamoto hizo anapaswa
kuzitatua ili kuweza kuleta hali ya upendo na amani katika vyama vya siasa.“Tumefurahi kupata msajili mpya wa
vyama vya siasa nchini, hivyo tunamuomba afanye kazi kwa ufasaha na kwa umakini
zaidi, ili kuweza kuondoa changamoto zilizopo katika mambo ya usajili wa
vyama,” alisema Nyambabe.
Aidha,
aliongeza kuwa Msajili mpya anapaswa kuboresha kanuni mbalimbali za usajili wa
vyama, kwani asilimia kubwa ya kanuni hizo zimepitwa na wakati na kanuni
nyingine hazioneshi wazi kuwa zinahitaji nini.
No comments:
Post a Comment