02 August 2013

WASIOONA WATAKA VIFAA VYA KUPIGIA KURANa Moses Mabula, Tabora
WATU wenye ulemavu wasioona mkoani Tabora wameiomba tume ya taifa ya uchaguzi kuwapatia vifaa maalum kwa ajili ya kupigia kura.Ombi hilo wamelitoa kwenye semina kati ya mashirika yasiyo ya kiserikali katika Manispaa ya Tabora na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kanisa la Moravian mjini Tabora.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa chama cha watu wasioona mkoani Tabora, Donatus Lupoli alisema kuwa tume hiyo ijipange, kuhakikisha kwamba watu wasioona wanapatiwa vifaa hivyo maalum ili nao waweze kushiriki kikamilifu katika zoezi la upigaji kura mwaka 2015.
Lupoli ameeleza kuwa walemavu hao hupata shida wakati wa zoezi la kupiga kura na kutoa wito kwa tume ya uchaguzi kuwa ni wakati umefika sasa kwa tume hiyo kufanya kila iwezavyo kuhakikisha kwamba kunawepo na vifaa hivyo maalum kwa ajili ya kupigia kura kwa watu wasioona.
Nae mwakilishi kutoka tume ya taifa ya uchaguzi, Batromayo Wandi amesema kuwa tume hiyo imeamua kuboresha Daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia mfumo wa Biometric.
Alisema kuwa mfumo huo una uwezo wa kuhifadhi hadi taarifa 12 na kwamba utaondoa mkanganyiko wa taarifa za mpiga kura.
Wandi alibainisha kuwa mfumo huo pia utasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa majina ya wapiga kura kujirudia katika Daftari hilo na kufanya kuaminika zaidi kwa wadau wa uchaguzi hapa nchini.
Alieleza kwamba mfumo huo hapa nchini utakuwa ni mchakato mpya wa uandikishaji wa wapiga kura kwa teknolojia mpya na kwamba maboresho hayo yanatazamiwa kuwa jibu la kanuni ya kura moja mtu mmoja kujirudia jina mara mbili katika Daftari la kudumu la wapiga kura

No comments:

Post a Comment