02 August 2013

SERIKALI YASITISHA UTOAJI VIBALI VYA KUISHI



 Na Theonestina Juma, Bukoba
UONGOZI wa Mkoa wa Kagera umesitisha utoaji wa vibali vya kuingia na kukaa nchini kupisha operesheni ya majambazi, wahamiaji haramu na wanaomiliki silaha kinyume cha sheria, ikiwa ni kutekeleza agizo ya Rais Jakaya Kikwete
.Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Mkoa Kagera, Kanali Fabian Massawe katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Bukoba.Alisema vibali hivyo vinasitishwa kutolewa na idara ya uhamiaji hadi pale msako huo utakapoisha.
Kanali Massawe alisema mbali na hiyo pia imetangaza donge nono kwa wananchi ambao watawapatia taarifa sahihi kwa wale ambao wanamiliki silaha kinyume cha sheria pamoja na wahamiaji haramu katika maeneo yao.Kanali Massawe alisema "kwa mtu yeyote atakaye tupa taarifa sahihi juu ya mtu ambaye anamiliki silaha kinyume cha sheria tutampatia sh. 100,000".
Alisema watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria wanatakiwa kuzisalimisha kwa viongozi wa kata, vitongoji, wenyeviti wa vijiji, tarafa, katika vituo vya polisi na hata katika ofisi ya mkuu wa mkoa."kwa sasa zimebaki takribani siku 10 msako huo kuanza, hivyo kwa yeyote asiyetaka kusalimisha silaha na hata yule mhamiaji haramu ambaye hataki kuondoka nchini kwa utaratibu asije akatulilia," alisema.
Alisema si kwamba Watanzania hawapendi wageni, lakini wanatakiwa kuingia nchini kwa kufuata utaratibu wa nchi husika, na si kuja kwa kujificha bali wanatakiwa kuja kifua mbele kwa kufuata sheria zilizopo.
Alisema ulinzi ni wa kila mmoja na ndiyo maana wanasisitiza ulinzi shirikishi na hii ni kutokana na polisi waliopo ni wachache na hivyo hawawezi kuachiwa wao peke yao.
Aidha alitoa tahadhari kwa wale wananchi wanaowahifadhi wahamiaji kuwa wakipatikana nao watafanywa kama wahamiaji haramu hao.
Julai 26, mwaka huu akiwa wilayani Biharamulo Rais Jakaya Kikwete alitangaza kuendeshwa kwa msako wa majambazi, wahamiaji haramu na wanaomiliki silaha kujisalimisha na kusalimisha silaha zao, ndani ya wiki mbili na baada ya hapo operetion kubwa itaendeshwa katika mikoa ya Kigoma, Kagera na Geita ya kuwasaka watu hao.
Rais Kikwete alitoa wiki mbili kwa watu hao kusamilisha silaha zao na wahamiaji haramu kuondoka nchini kwa amani kwa sababu nchi haiwezi kubadilishwa shamba la bibi la kila mtu anaingia anavyotaka bila kufuata utaratibu wa nchi husika.
Alisema katika msako huo unaotarajiwa kuanza, utashirikisha vyombo vyote vya majeshi, wakiwemo JWTZ na usalama wa taifa

No comments:

Post a Comment