28 August 2013

UTUPAJI TAKA HOLELA WAMPANDISHA KIZIMBANI MTU mmoja mkazi wa Mtoni, Wilaya ya Temeke amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Jiji Sokoine Drive kwa kosa la kutupa takataka eneo lisilo rasmi, anaripoti Revina John.

Mwendesha Mashtaka, William Mtaki, alidai mbele ya Hakimu John Kijumbe, kuwa mtuhumiwa Amiri Hashimu (35) mkazi wa Mtoni, alikutwa maeneo ya Temeke Buza akitenda kosa hilo.Mtaki alisema kuwa, mtuhumiwa alitenda kosa hilo Agosti 25, mwaka huu,saa 10:00 jioni maeneo ya Temeke Buza jijini Dar es Salaam.
Mtuhumiwa alikana shtaka ambapo dhamana yake ni sh. 500,000 ikiwa ni pamoja na wadhamini wawili, ambao watakuwa na barua kutoka kwa wajumbe wao. Kesi hiyo itatajwa tena Septemba 10, mwaka huu.Wakati huo huo, Ramadhani Omary (38) na Juma Salum (25) wakazi wa Dar es Salaam, wamepandishwa kizimbani katika mahakama hiyo kwa kosa la kufanya biashara eneo lisilo rasmi.
Ilidaiwa na Mwendesha Mashtaka, Richard Magodi, mbele ya Hakimu, Timothy Lyon, kuwa watuhumiwa walitenda kosa hilo Agosti 26, mwaka huu, katika eneo la Posta Wilaya ya Ilala.Magodi aliendelea kudai kuwa watuhumiwa walikutwa wakiuza nguo pamoja na pipi eneo hilo. Kesi yao itatajwa tena Septemba 6, mwaka huu na dhamana yao iko wazi..

No comments:

Post a Comment