16 August 2013

VIINGILIO YANGA,AZAM VYATANGAZWANa Amina Athumani
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetangaza viingilio vya mechi ya Ngao ya Jamii kati ya mabingwa waetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga dhidi ya Azam FC, itakayochezwa kesho kutwa uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema viingilio katika mechi hiyo cha chini kitakuwa sh. 7,000 na cha juu ni sh. 30,000.Alisema kiingilio cha sh. 7,000 ni kwa viti vya rangi ya kijani na bluu wakati viti vya rangi ya chungwa ni sh. 10,000, VIP C watalipa sh. 15,000, VIP B sh. 20,000 na VIP A watalipa sh. 30,000.
Wambura alisema mechi hiyo ni ya Ngao ya Jamii na kuashiria uzinduzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu kwa mwaka 2013/2014.Alisema mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni ambapo mshindi atakabidhiwa ngao.
Wambura alisema iwapo dakika 90 za mechi hiyo hazitatoa mshindi, timu hizo zitatenganishwa kwa mikwaju ya penalti.Alisema mbali na mechi hiyo kuashiria uzinduzi wa msimu wa ligi, pia mapato yanayopatikana yatasaidia mambo mbalimbali ya kijamii.
Ofisa huyo alisema kwa mwaka huu asilimia 10 ya mapato ya mechi hiyo, yatapelekwa kwenye kituo cha kulelea watoto cha SOS.Wambura alisema katika mechi ya Ngao ya Jamii mwaka jana, asilimia 10 ya mapato yake yalipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke, ambapo walinunua kitanda cha kufanyia operesheni kwa wagonjwa wa upasuaji.

No comments:

Post a Comment