07 August 2013

UTEKAJI WA DKT. ULIMBOKA:SIRI NZITO YAFICHUKA


Na Rehema Mohamed
MKURUGENZI wa Mashtaka Nchini (DPP) amemfutia mashtaka raia wa Kenya, Joshua Muhindi (22) aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya kumteka na kumdhuru Dkt.Steven Ulimboka na kisha kumfungulia shtaka jipya la kutoa taarifa za uongo kwa Jeshi la Polisi.Mshtakiwa huyo jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu

Waliyarwande Lema ili upande wa mashtaka ueleze mustakabali wa kesi hiyoHata hivyo, Wakili wa Serikali Beata Kitau aliieleza mahakama hiyo kuwa DPP hana nia ya kuendelea na shauri hilo dhidi ya mshtakiwa hivyo anaomba kuliondoa chini ya kifungu 91(1) cha Mwenendo wa Makosa ya jinai (CPA).
Hakimu Lema alikubaliana na hoja hiyo na kuifuta kesi hiyo ambapo hata hivyo baada ya kutoka mahakamani mshtakiwa huyo alikamatwa tena na polisi na kisha kupandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Aloyce Katemana.
Akiwa mbele ya hakimu huyo, wakili wa serikali Tumaini Kweka alimsomea shtaka la kutoa taarifa za uongo kinyume na kifungu 122 cha kanuni ya adhabu sura ya 16.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, Julai 3, 2012 Kituo cha Polisi Oysterbay mshtakiwa huyo (Muhindi) alitoa taarifa za uongo kwa ofisa wa Polisi kwamba yeye na wenzake wasiojulikana walimteka na kumjeruhi Dkt. Ulimboka wakati akijua si kweli.
Mshtakiwa huyo alikana kutenda kosa hilo ambapo upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika na wanaomba tarehe ya kutajwa ili wamsomee maelezo ya awali.
Baada ya kusema hivyo, Muhindi aliiomba mahakama impe dhamana na kwamba alikuwa na wadhamini, lakini hata hivyo upande wa mashtaka ulipinga kwa madai kuwa mshtakiwa ni mgeni na hana makazi maalumu hivyo itakuwa vigumu kumpata.
Hata hivyo, Mkenya huyo aliibuka na kudai kuwa amekaa gerezani toka Julai 13, 2012 lakini upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake hadi jana wanamfungulia mashtaka mengine.
Alidai kuwa jambo la kumrudisha yeye gerezani linalenga kumpoteza ili kutuliza umma na Bunge na kwamba akirudi gerezani atagoma na kufanya maandamano.
“Hawa watu wanataka kunipoteza mimi kijana mdogo wa miaka 22, mashtaka wanayonishtakia si ya kweli naumia sana hakimu, nikirudi gerezani nitafanya maandamano na kugoma, hakimu utapata taarifa,” alidai Muhindi.
Kwa upande wake Hakimu Katemana aliutaka upande wa mashtaka kuwasilisha mahakamani hapo hati ya zuio la dhamana kama wanataka mshtakiwa huyo asidhaminiwe kwa sababu shtaka analokabiliwa nalo linadhaminika.
Alimweleza mshtakiwa huyo kuwa atakuwa nje kwa dhamana ikiwa atatimiza sharti la kuwa na wadhamini wawili kutoka taasisi zinazotambulika watakaosaini bondi ya sh. milioni tano na pia awasilishe mahakamani hapo hati zake za kusafiria.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 20 mwaka huu

5 comments:

  1. NADHANI SASA POLISI WANALO JINA LA MTU AU WATU WALIOMTEKA ULIMBOKA

    ReplyDelete
  2. danganya toto hiyooooooo!!!!!!!!!!!!!.........

    ReplyDelete
  3. Kwanini hao mapolisi wa Tanzania wanazidi kubobea kusema uwongo! Kwani hawajui mhusika wa unyama aliofanyiwa Dr. Ulimboka? Hebu acheni kuliaibisha taifa na hizi "danganya toto" za kila siku. Au hapo ndo utaalamu wenu umefikia! Hamuwezi kwenda zaidi!!!

    ReplyDelete
  4. KESI IKISHAANZA KUZUNGUMZIWA MAGAZETINI NI KUHARIBU MWENENDO WA KESI HAKUNA HAKI TENA KAMA BUNGENI HAWARUHUSIWI KUZUNGUMZIA MASUALA YA MAHAKAMANI MBONA MAGAZETI HAWAZUILIWI KATIBA MPYA IWAFUNGE MIDOMO

    ReplyDelete
  5. This is one of the reasons to, why our Country is now Politically Unstable. Serikali isome alama za nyakati

    ReplyDelete