- WATENDAJI WATUHUMIWA KUTAFUNA MAMILIONI YA KODI MIAKA 30
- MADIWANI,DED WASHANGAA FEDHA ZILIKO WAUNDA TUME MAALUM
Na
Mwandishi Wetu, Mbozi
MAMILIONI
ya fedha za Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya yanayotokana na pango
la nyumba tatu za halmashauri hiyo yanadaiwa kutafunwa na watendaji kwa miaka
30 iliyopita.watendaji wanatuhumiwa kuficha vyanzo vya
mapato hayo kwa nia ya kujinufaisha wenyewe.
Hoja hiyo
iliibuliwa mwishoni mwa wiki katika kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri
hiyo na Diwani wa Kata ya Ihanda, Joel Kasebele (CCM) wakati wa maswali ya papo
kwa papo kwa Mkurugenzi wa halmashauri, Levison Chilewa ambaye alitakiwa kutoa
ufafanuzi juu ya mahali zinapokwenda fedha za pango za nyumba tatu.
Diwani huyo
alisema, nyumba hizo zimepangishiwa watu na taasisi binafsi za Tanganyika
Farmers Association (TFA), Chama cha Akiba na Mikopo karibu na soko la Vwawa na
nyumba ya kulala wageni ya Mbozi Development Council (MDC) ambazo tangu
zilipopangishwa mwaka 1983 hakuna mapato yaliyoingizwa kwenye halmashauri hiyo.
"Mheshimiwa
Mwenyekiti napenda kupata ufafanuzi juu ya mapato ya fedha zinazotokana na
nyumba tatu zinazomilikiwa na halmashauri yetu, zinakwenda wapi? Nyumba hizo ni
za halmashauri mapato yake yanafanya kazi gani?” alihoji Kasebele.
Akijibu hoja hiyo, Mkurugenzi wa
halmashauri hiyo, Chilewa alisema kuwa hajui fedha za nyumba hizo zinakokwenda
na kwamba tangu ameingia hapo miaka saba iliyopita hajawahi kupewa taarifa
kuhusu mapato ya nyumba hizo na kwamba hata hivyo ofisi yake imewaandikia barua
wapangaji ili kujua mkataba wa upangaji wa nyumba hizo.
"Lazima niseme ukweli hili jambo
nimelikuta, sijui lolote kuhusu mapato ya nyumba hizo, tangu nimefika miaka
saba sasa sijapewa mrejesho wowote kuhusu nyumba hizo," alisema Chilewa.
Kufuatia majibu hayo baadhi ya madiwani
walisimama ili kupata ufafanuzi zaidi na kuhoji sababu za ofisi ya halmashauri
hiyo kuachia mapato ya nyumba hizo kwa takriban miaka 30 bila kufuatiliwa.
Alisema kuwa, siku za nyuma hakukuwa na
kumbukumbu wala taratibu zozote za vyanzo vya mapato kutoka kwa uongozi
uliopita na kwamba nyumba hizo zimeibuliwa hivi karibuni ambapo jitihada
zinafanyika ili kujua mikataba ya wapangaji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri
hiyo, Elick Ambakisye alisema kuwa kikao cha Baraza la Madiwani kimeiagiza
ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuandaa taarifa sahihi ya kina juu ya
vyanzo vingine vya mapato ambavyo fedha zake zinaingia mifukoni mwa wachache.
Mwenyekiti huyo alisema, wanasubiria kutoa
uamuzi wao juu ya kinachoendelea kuhusiana na tukio hilo katika kikao cha
Baraza la Madiwani kinachotarajiwa kukutana Agosti 14, mwaka huu.
Hata hivyo, awali ilidaiwa kuwa, baadhi ya
watendaji wa halmashauri hiyo wamekuwa wakichukua kodi katika nyumba tatu za
halmashauri hiyo bila kuziwasilisha ofisini huku wengine wakijimilikisha nyumba
hizo na kufahamika kwa wapangaji kama ni wamiliki wa nyumba hizo.
Wakati huo huo, jitihada za kuwatafuta wapangaji wa nyumba hizo ili kupata taarifa za
kodi wanazolipa kila mwezi zinaendelea baada kufuatiliwa muda mrefu bila
mafanikio.
MIAKA THELASINI MULIKUWA WAPI JE NI KUONYESHA IWAPO MUNAFANYA KAZI MUTAPIMWA UCHAGUZI UJAO IWAPO MUTAGOMBEA KWA KATIBA MPYA
ReplyDelete