06 August 2013

TENDWA ANG'ATUKA APATA MRITHI WAKE

Na Goodluck Hongo
RAIS Jakaya Kikwete, amemteua Jaji Francis Mutungi, kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa.Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na kusainiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, imeeleza kuwa uteuzi huo ulianza Ijumaa, Agosti 2, 2013.Jaji Mutungi anachukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, ambaye amestaafu Utumishi wa Umma kwa mujibu wa sheria.
Kabla ya uteuzi huo, Jaji Mutungi alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma

.Wakizungumzia mabadiliko hayo, baadhi ya wanasiasa siasa wamefurahishwa na kustaafu kwa, Tendwa, kwa kile walichodai uongozi wake alichangia kukandamiza demokrasia nchini.Kwa upande wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema Bw John Tendwa alitakiwa awe ameondoka kwenye Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa, tangu mwaka 2008, alipofikisha umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria, lakini mkataba wake alioongezewa kwisha, kuwa mwisho wake umefika.Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na ofisa habari wa Chama, Tumaini Makene, alisema ametumia muda huo mwingi kwenye ofisi ya umma kinyume cha sheria.Alisema kutokana na mwenendo wake mbovu, CHADEMA ilitangaza kutompa ushirikiano wowote.
Alisema kwa muda wote huo, CHADEMA ilikuwa ikitoa ushirikiano kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, lakini si kwa Tendwa. Alisema badala ya kuifuta CHADEMA ameondoka yeye.
Alisema kuondoka kwa Tendwa hakuzuii kutekelezwa kwa mapendekezo ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, iliyomkuta na hatia ya kuvunja Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Sensa, hadi yakatokea mauaji ya Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi, Nyololo, Iringa.
Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP) Augustino Mrema, alisema Tendwa, ndiye alifikisha chama cha NCCR-Mageuzi, hapo kilipo, hivyo anampongeza Rais Kikwete kwa kumteua Jaji Mutunga, kwani atatenda haki kama alivyokuwa akitenda haki mahakamani.
“Tendwa alikuwa kero kwa vyama vingine vya siasa kikiwemo chama changu cha NCCR-Mageuzi (wakati ule) mfano CCM ina vikundi vya majeshi, lakini CHADEMA ikitangaza kuanzisha vikundi hivyo anakuwa mkali. Alidai kuwa upendeleo wa Tendwa, ndiyo ulimfanya aendelee kushika wadhifa huo.
Naibu Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Abdul Kambaya, alisema chama chake kimefanya kazi na msajili huyo, lakini alikuwa na kasoro na alishindwa kuchukua hatua kwenye baadhi ya matukio.
Alitolea mfano mauaji ya Arusha, Arumeru, Igunga watu kumwagiwa tindikali, ikiwemo baadhi ya viongozi kuonesha bastola hadharani, lakini alishindwa kuchukua hatua dhidi yao.
“Tunapokea uteuzi wa Jaji Mutunga, lakini angalizo letu kwake ni lazima awe na nguvu ya kutoa adhabu kwa vyama vyote si kama alivyokuwa Tendwa.” alisema Bw. Kambaya
Naye Mwenyekiti wa Chama cha APPT-Maendeleo, Peter Mziray, alisema wao wanampongeza Tendwa kwa kazi nzuri aliyoifanya na wanamtakia mapumziko mema huko mtaani.

No comments:

Post a Comment