HIVI karibuni
Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilitangaza na kutoa
takwimu kuhusu wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano katika
shule za Serikali na vyuo vya ualimu kwa mwaka huu.Katika taarifa
hiyo ya Serikali ambayo ilionesha kuwa kutakuwa na upungufu mkubwa wa wanafunzi
10,074 katika sekondari 207 zinazomilikiwa na Serikali.
Taarifa hizi
hazishangazi sana kutokana na matokeo mabovu ya wanafunzi wa kidato cha nne
katika mwaka uliopita. Kwani katika matokeo hayo wanafunzi zaidi ya asilimia 60
walifeli mitihani yao na hivyo kuwa gumzo na simanzi kwa serikali, wazazi,
wanafunzi, wananchi na Taifa kwa ujumla wake .
Hali katika
sekta ya elimu nchini imezidi kuonesha kudidimia kwani kiwango hicho cha kufeli
hakikuwahi kutokea katika historia ya nchi yetu.
Kama tujuavyo
elimu ni suala mtambuka na linagusa karibu kila sekta nchini ikiwamo sekta ya
elimu yenyewe, kilimo na madini. Hivyo kama Serikali itaendelea kufumbia macho
elimu ya nchi hii, Taifa halitakuja kupiga hatua ya kimaendeleo katika miaka
nenda rudi.
Kutokana na
takwimu hizo zilizotolewa na Serikali ambapo imeonesha upungufu mkubwa wa
wanafunzi katika shule zinazomilikiwa na Serikali, lakini pia bado athari ya
takwimu hizi itaenda mpaka kwenye vyuo vya juu kwa kukosa wanafunzi kwa ajili
ya masomo ya ngazi mbalimbali za elimu.
Pamoja n a hayo S e r i k a l i imeshindwa
kuongeza shule kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano kutokana na sababu
hiyo hiyo ya upungufu wa wanafunzi katika shule za Serikali. Kitu
kilichonipelekea kuandaa makala haya.
Serikali pia imeshindwa kuongeza shule kwa
sababu ambayo ukiiangalia ni ya wazi kabisa ya upungufu uliopo wa wanafunzi
lakini nadhani sababu hii si ya msingi sana, kwani upungufu wa wanafunzi kwa
mwaka huu haumaanishi itakuwa hivyo mwakani na miaka mingine inayokuja.
Upo msemo hapa unaosema 'bora kuwa nacho
kuliko kukosa kabisa', msemo huu una maana kubwa katika hali tuliyonayo. Ni
kweli kutokana na matokeo ya kidato cha nne na wanafunzi waliochaguliwa
kujiunga na shule hizo za Serikali zilizopo kuna upungufu mkubwa sana wa
wanafunzi katika shule zinazomilikiwa na Serikali.
Lakini hili lisizuie Serikali kujenga
shule zingine kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano, kwani takwimu hizi
zinaweza kubadilika mwakani au katika mwaka wowote ule.
Serikali kupitia kwa Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi inapaswa kuongeza shule kwa wanafunzi wa kidato cha tano
vilevile kwa wanafunzi wa vidato vya chini.
Kujengwa kwa shule hizi kunaweza kusaidia
baadaye hasa katika kudahili wanafunzi wachache watakaokidhi katika kila shule
kutokana na idadi ya wanafunzi waliofaulu.
Lakini pia hali ya ufaulu inaweza
kuongezeka katika mwaka ujao wa masomo au katika miaka mingine na hivyo kukawa
na tatizo la wanafunzi kukosa shule hii inawezekana kabisa na kama Serikali
itakaa na ikadhani kwamba ufaulu wa wanafunzi utaendelea kushuka basi hali
inaweza kuwa mbaya zaidi ya wanafunzi kukosa shule.
Mara nyingi walimu wamekuwa wakilalamika
wanafundisha wanafunzi wengi tofauti na namba halisi inayopaswa kuwepo darasani
lakini kwa hali ilivyo sasa kwa wanafunzi wa kidato cha tano itabadilika kwani
wanafunzi ni wachache ukilinganisha na shule zilizopo.
Wasiwasi wangu ni vipi hali ya mambo
itakapobadilika, kwani zipo juhudi za wazazi,walimu na wanafunzi za kutaka
kubadilisha hali ya elimu nchini kutokana na matokeo na takwimu hizi mbovu.
Nafikiri ni vyema kwa Serikali kulingana
na bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kujenga shule za kutosha za
kidato cha tano kwa ajili ya wanafunzi wa miaka inayofuata.
Kama nilivyosema awali ni vyema ukawa
nacho kuliko kukosa kabisa, hivyo nazidi kuishauri Serikali kuwa ni bora kuanza
mipango ya mapema ya kuongeza shule za kidato cha tano badala ya kungoja
ongezeko la ufaulu ndipo waanze na mikakati hii.
Serikali ina jukumu kubwa la kuleta
mabadiliko ya sekta ya elimu nchini na likiwemo hili jukumu la kujenga shule za
sekondari, vyuo vya ualimu, vyuo vya ufundi na vyuo mbalimbali vya elimu ya
juu.
Hivyo basi kulingana na bajeti ya wizara,
Serikali ingepaswa kuongeza shule kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano,
Serikali inapaswa kutekeleza azma hiyo kwani pamoja na matokeo na takwimu
zilizotolewa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi bado kuna nafasi ya
mabadiliko makubwa katika miaka inayofuata.
Ipo dhana kwamba kutokana na mfumo wetu wa
elimu kuna hatari kubwa ya kuendelea kuporomoka kwa viwango vya ufaulu kwa
wanafunzi wa kidato cha nne, na kimsingi kabisa nakubaliana nayo, lakini
wasiwasi wangu ni vipi hali ikibadilika? Ni vipi katika mwaka huu wanafunzi wa
kidato cha nne wakafanya vizuri zaidi katika mitihani yao? Rai yangu kwa
Serikali ni kujenga shule zakutosha zenye lengo la kudahili wanafunzi wa kidato
cha tano.
Mwandishi wa makala haya ni mwanahabari na
mwanafunzi wa Stashahada ya Sheria katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama- Lushoto
No comments:
Post a Comment