06 August 2013

UVUVI HARAMU WAATHIRI MAPATO YA HALMASHAURI


Na Jovither Kaijage, Ukerewe
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza wamekumbushwa kuchukua hatua za haraka kuzuia uvuvi haramu unaozidi kushamiri ili kuokoa uchumi wake ambao kwa zaidi ya asilimia 80 unategemea sekta hiyo
.Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Joseph Mkundi, aliliambia Baraza la Madiwani jana kuwa tatizo hilo lisipodhibitiwa haraka litasababisha halmashauri hiyo ishindwe kutoa huduma za kijamii.
Akijibu hoja za kamati ya madiwani wa CCM zilizowasilishwa na diwani wa Kata ya Kakerege, Juma Mazigo, alisema taarifa za idara ya uvuvi zilizopo zinaonesha hali ya upatikanaji wa samaki inashuka.
Akifafanua zaidi alisema mwaka 2009 katika wilaya hiyo zilivuliwa tani 25,400 za samaki aina ya sangara, mwaka uliofuata tani 21,000 na hali iliendelea kuwa mbaya zaidi, ambapo mwaka 2011 zimevuliwa tani 13,000 tu.
Alibainisha kuwa upatikanaji wa samaki aina ya sato umeshuka kutoka tani 9.8 mwaka 2009 hadi tani 3.9, huku mwaka 2010 zikivuliwa tani 7.2 na kuongeza kuwa samaki aina ya dagaa mwaka 2009 zilivuliwa tani 67 mwaka uliofuta tani 51 na mwaka 2011 zikavuliwa tani 30 pekee.
Kutokana hali hiyo, aliwataka madiwani hao kutambua kuwa hakuna njia nyingine ya kuinua mapato ya halmashauri ya wilaya hiyo kama wasipotokomeza uvuvi haramu ambao ndio sababu kubwa ya kupungua samaki katika ziwa hilo.
Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, Mery Tesha, ameliambia baraza hilo la madiwani kuwa tatizo hilo la uvuvi haramu limefikia hatua mbaya zaidi baada ya hivi karibuni kukamatwa lita tatu za sumu aina ya Thiodani katika kata ya Ngoma iliyoandaliwa kutumika kuulia samaki katika ziwa hilo.
Hata hivyo, mbali na kuwataka madiwani kushiriki hasa ni kuwaelimisha wananchi madhara ya tatizo hilo pia amesema tayari ameagiza misako iendeshwe kwa kila kijiji cha wilaya hiyo ili kupunguza tatizo hilo. 

No comments:

Post a Comment