OFISA Mfawidhi wa Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA)
mkoani Iringa, Rahim Kondo amesema mamlaka hiyo katika Manispaa ya Iringa
imeongeza vituo vya mabasi.Lengo likiwa ni kuondoa msongamano katika Kituo cha Mabasi Miyomboni
ambacho kilionekana kuelemewa kabla ya kufungua stendi nyingine nne na
kuwezesha wananchi sasa kupata usafiri kwa urahisi zaidi kuliko hapo awali
ambapo walikuwa wanakaa muda mrefu kusubiria daladala zipakie hadi zijae ndipo
waondoke.
Akizungumza na Majira ofisini kwake jana, ofisa huyo alisema vituo vya
mabasi ambavyo vimeongezwa ni pamoja na Kituo cha Mashine Tatu ambacho
kitatumika katika kupakia na kushusha abiria wa daladala za Cgrielo Mashine
Tatu, Kiwandani kuja Mashine Tatu na daladala za kwenda Igumbilo kuja Mjini
ambapo zitatakiwa kuishia Mashine Tatu.
Alifafanua kuwa, katika kituo cha Mlandege daladala zitapakia na
kushusha kutoka Nyabula kuja Iringa Mjini, kituo cha MR Hotel kitatumiwa na
daladala za kutoka Mawelewele kuja Mjini, Don Bosco kuja Mjini, kutoka Megic
Site kuja Mjini ambapo kituo kipya cha eneo la Posta kitatumika kwa daladala
ambazo zinafanya safari ya kutoka Kalenga kuja Mjini na Ipamba kuja Mjini.
Pia amewataka
madereva wahakikishe wanazingatia ruti zao bila kuzivuruga.
Akizungumzia
sababu ya kuongezwa kwa vituo hivyo, Kondo alisema kuwa abiria walikuwa
wanalazimika kusafiri na kulipa nauli zaidi ya mara mbili hadi tatu hali ambayo
kwa sasa itawawezesha kutumia nauli moja kufika mjini na hatimaye kuendelea na
shughuli zao ambazo wanataka kuzifanya.
"Vituo
hivi...kwa kweli vinalenga kupunguza msongamano, kuboresha usafiri kwa abiria,
hadi sasa tunafanya uchunguzi wa maeneo mengine ambayo daladala hazifiki
tutapima kilomita na tutazisajili daladala zifanye safari zao huko na maeneo
yote ya mji wa Iringa tunataka kuhakikisha kunakuwepo usafiri kila wakati ili
wananchi watumie muda wao vizuri kufanya shughuli na siyo kukaa kwenye vituo
vya mabasi kwa muda mrefu," alisema ofisa huyo wa SUMATRA.
Aliongeza kuwa,
suala la kuongeza vituo hivyo vipya limewezesha kupunguza foleni ya kukaa muda
mrefu katika kituo kimoja huku daladala zikisubiriana zijaze ambapo kwa sasa
kila daladala zitafanya safari kutoka eneo ambalo zimesajiliwa hadi kituo
kimoja na kugeuka mara moja.
Hali ambayo
itawasaidia abiria huku ikiwaongezea kipato wamiliki wa mabasi na daladala na
kutumia muda vizuri.
No comments:
Post a Comment