12 August 2013

TAASISI ZA FEDHA ZAHIMIZWA KUACHA URASIMU KATIKA MIKOPO



Na Esther Macha, Mbeya
TAASISI za fedha zimetakiwa kuwa rafiki wa mkulima kwa kuwapatia mikopo ili kuwaondolea usumbufu ambao wamekuwa wakipata.Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu, wakati alipotembelea mabanda ya wakulima katika Maonesho ya Wakulima Nane nane yaliyofanyika katika viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.

Mkuu huyo wa mkoa alisema baadhi ya taasisi za fedha zimekuwa na kasumba mbaya kwa wakulima ambapo zimekuwa zikiwabagua pindi wanapofika kuomba msaada wa kukopeshwa.Mwambungu alisema wafanyakazi wa mabenki na taasisi zingine za fedha wanatakiwa kuwa karibu na wakulima hao pia watumie zaidi taaluma na uzoefu wao kuwasaidia ili waweze kuinuka kiuchumi.
Alisema mabenki na taasisi za kifedha zinatakiwa kuondokana na kasumba kuwa hawana uwezo wa kurejesha mkopo badala ya kuthamini wafanyabiashara pekee. “Wakati wakipewa elimu ya matumizi sahihi ya fedha wanazokopeshwa wanakuwa na uwezo mzuri wa kurejesha,” alisema na kuongeza;
“Mkulima apewe elimu na taasisi hizo juu ya ureshaji wa fedha anazokopa, hapo atakuwa mrejeshaji mzuri wa fedha hizo.”Alisema mkulima bila ya kusaidiwa kwa vitendea kazi ataendelea kupiga hatua moja mbele na kurudi hatua tatu nyuma, badala ya kusonga mbele.
Alisema maonesho ya wakulima hayana maana kama hawatapewa msaada wowote hususani kutoka taasisi za fedha kwa kuwapatia mawazo ya kuwawezesha kusonga mbele zaidi kiuchumi

No comments:

Post a Comment