12 August 2013

WAKULIMA WATAKIWA KUTONUNUA PEMBEJEO PASIPO KUSHAURIWA



 Na Esther Macha, Mbeya
WAKULIMA mkoani Mbeya wameshauriwa kutonunua pembejeo za kilimo kwenye kampuni zinazozalisha mbegu kabla ya kupatiwa ushauri wa wataalamu wa kilimo.Hatua hiyo inatokana na wakulima wengi kujenga utamaduni wa kwenda kwenye kampuni zinazozalisha pembejeo na kununua mbegu bila kujua matumizi yake na matokeo yake kuvuna mazao ambayop hayalingani na mashamba yao
. Mwito huo ulitolewa hivi karibuni na Meneja Masoko wa Kampuni ya TANSEED International, Safiel Msovu, wakati akizungumza na gazeti hili katika maonesho ya wakulima ya Nane nane ambayo yalifanyika katika viwanja vya John Mwakangale mjini hapa.Hata hivyo, Msovu alisema kama kampuni hawana utaratibu wa kuuza mbegu kiholela kwa wakulima na kwamba wanachofanya wao ni kutoa elimu kwanza juu ya matumizi ya mbegu hizo kwa mkulima ili aweze kufahamu mbegu ipi inafaa kupandwa wapi kwa kuzingatia hali ya hewa.
“Sisi kama wataalamu tunafahamu kuwa mkulima ikifika kipindi cha msimu wa kilimo anakuwa na haraka ya kuwahi msimu wa kilimo, hivyo anaishia kununua mbegu ambayo si bora,”alisema Msovu.
Meneja huyo alisema ili wakulima waweze kuzalisha mazao mengi, wanashauriwa kufika kwenye ofisi za TANSEED ili wapatiwe ushauri wa kutumia mbegu bora kutoka kwa wataalamu.
“Tunashauri watumie mbegu ya TAN 222 ya mahindi, TAN H 600 ya mpunga TXD 306, SARO5 hii ni bora kwa mkulima yeyote,”alisema.
Kwa upande wake Meneja Uzalishaji wa Kampuni hiyo, Happy Shuma, aliwataka wakulima pindi wanaponunua mbegu kwenye kampuni kudai stakabadhi ambayo itawasaidia kujua kama mbegu waliyonunua haitakuwa na ubora, hivyo kuwa rahisi kufika katika kampuni husika kulalamikia.
“Kudai stakabadhi ni haki kwa kila mkulima kwani hiyo itakuwa msaada kwake hata kutambua ubora wa mbegu alikonunua na hata kama kuna tatizo linalohusiana na masuala ya kilimo,” alisema.
Mmoja wa wakulima walioshiriki maonesho hayo, Atumanyise Peter, alisema wakulima wengi wamekuwa wakinunua bila kufahamu matumizi ya mbegu hizo, hivyo ni jukumu la kampuni husika kuhakikisha zinatoa elimu kabla mkulima hajanunua mbegu hizo.

No comments:

Post a Comment