02 August 2013

SHERIA YA MATUNZO IONGEZWE MAKALI KUWABANA WANAOTELEKEZA FAMILIAReuben Kagaruki
MIMI kutolala na mke wangu kunatokana na yeye kuninyima tendo la ndoa..., kila ninapolala kwake nakuwa kama niko kwenye lindo, hanipi unyumba kabisa, kamwe sikubali. Kama mwenzangu ana mahali anakomalizia shida yake, basi aseme
.Kauli hiyo ni ya mkazi wa Kata ya Nachingwe wilayani Ruangwa, Mohamed Said Ndende, ambayo aliitoa mbele ya Mtendaji wa Kata ya Nachingwe wilayani Ruangwa Rajab Macholilo, akizungumzia mgogoro wake na mkewe.
Ndende anasema amekuwa akimsaidia kulima isipokuwa anachodai, Darlin Hassan (mke wake) maarufu kwa jina la Bibi Dogo labda ni suala la ngono tu yaani kutotimiziwa tendo la ndoa.
Ndende, anakiri kwamba Bibi Dodo ni mkewe na wameishi naye kwa miaka mingi. Akitoa ushuhuda wa tukio la kutelekezwe na mume wake, Bibi Dogo anasema;
“Nimezaa na mume wangu huyo (Ndende) watoto watano na sasa hivi ni wakubwa. Tumeishi naye kwa zaidi ya miaka 40. Wazee wametukalisha vikao kadha wa kadha wakimsihi anihudumie mimi na watoto wetu hao, lakini hafanyi hivyo, tabia yake haibadiliki.
L a k i n i s i w e z i kumfunga ninachohitaji ni haki yangu tu,” anasema Darlin kwa masikitiko.
Anaongeza kuwa: “Aliwaambia ndugu zangu eti amepata mke mwingine. Mpaka sasa tuko wake watatu, mke wake wa pili alifariki na sasa anaishi na mke wake wa tatu.
Nimemwambia tukakae wote huko, lakini hataki...namtaka anitimizie mahitaji yangu ya ndani na anisaidie kulima, lakini hataki,” alizidi kulalamika.
Kilio cha mwanamke huyo ni kielelezo cha matatizo yanayotokea ndani ya ndoa hadi kufikia hatua ya wanawake kutelekezwa na kujikuta wakibaki na jukumu la kutunza familia.
Hali hiyo inatokea hapa nchini ikieleweka wazi kuwa wanaume ndiyo nguzo ndani ya familia yoyote. Mara nyingi nguzo hiyo muhimu ndani ya familia inaposhindwa kutimiza wajibu wake familia inayumba na kupoteza mwelekeo.
Leo hii watoto wengi wanaishi katika mazingira magumu kutokana na wanaume kushindwa kutimiza wajibu wao. Tatizo hili ingawa linachangiwa na vifo, lakini kwa upande mwingine linachangiwa na wanaume kutelekeza familia zao.
Mfano, kati ya kesi zinazoongoza kwenye mabaraza ya usuluhishi kwenye kata ni zile za wanaume kutelekeza familia. Mara nyingi inapotokea migogoro kwenye familia waathirika wakubwa ni wanawake na watoto.
Utafiti uliofanywa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na Kituo cha Usuluhishi cha TAMWA (CRC) kwenye mpango wa kutokomeza ukatili na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto (GEWE II) katika wilaya 10 za Tanzania bara na Zanzibar umeweza kubaini ukubwa wa tatizo la wanaume kutelekeza wanawake na watoto.
Wilaya za Utafiti zilikuwa ni Wete, Unguja Mjini Magharibi na Unguja Kusini.
Zingine ni Kinondoni na Ilala Kisarawe, Mvomero, Ruangwa na Lindi Vijijini na Newala.
Utafiti umeonesha wazi kuwa moja ya matukio ambayo yanayoonekana kushamiri katika jamii ni wanaume kutelekeza wanawake zao na watoto.
Kwa mujibu wa utafiti, sababu zinazowafanya wanaume watelekeze wake wao ni kukosa uaminifu, ugomvi usioisha na maisha magumu hasa pale wilaya ama eneo husika linapokumbwa na baa la njaa.
Utafiti umebaini kuwa tatizo hili lipo katika wilaya zilizofanyiwa utafiti yaani tatu za Zanzibar na saba za Tanzania Bara.
Baadhi ya sababu zinazochangia ni kutotumika ipasavyo kwa sheria zinazaowalinda wanawake na watoto kama sheria ya mtoto ya mwaka 2009, jamii kutokuwa na elimu ya ndoa hivyo wanaume kuutumia vibaya uongozi ndani ya familia zao, vipigo ndani ya ndoa, rushwa kutawala katika vyombo husika, kukosekana uaminifu ndani ya ndoa talaka na kupotea kwa maadili katika jamii.
Athari za wanawake na watoto kutekelezwa, ni watoto kukosa malezi ya wazazi wawili, kuacha masomo kutokana na ugumu wa maisha na kulazimika kuingia kwenye ajira mbaya ikiwemo uasherati na kazi ngumu kama vile kupasua kokoto ili kuingiza kipato katika familia zao.
Aidha, wanawake kubebeshwa mzigo mkubwa wa kutunza familia na kuwafanya kurudi nyuma kimaendeleo, kuongezeka umaskini, familia kusambaratika na wanawake kukosa haki zao.
Katika wilaya tatu za Zanzibar, jumla ya matukio ya utelekezwaji wanawake ni kama ifuatavyo; Katika Wilaya ya Wete kulikuwa na 131, Magharibi 239, Kusini Unguja 11. Chanzo cha takwimu hizo ni Dawati la Jinsia.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa baadhi ya waathirika hawaripoti matukio ya udhalilishaji katika mamlaka husika na hivyo takwimu kuonesha matukio hayo ni machache.
Utafiti huu pia umebaini kuwa talaka zimechangia kwa kiasi kikubwa wanawake na watoto kutelekezwa. Jeshi la Polisi Pemba, limethibitisha kuwa tatizo ni kubwa kutokana na waathirika kutoripoti matukio katika vyombo vya sheria.
Kwa mfano, jeshi hilo limesema mwaka 2011, Dawati la Wanawake na Watoto la Polisi Kaskazini Pemba, lilipokea jumla ya kesi nane ambapo mwaka 2012 kesi sita na kipindi cha Januari hadi Machi, 2013 ni tukio moja tu lililoripotiwa.
Lak in i taar if a za wizar a zimebainisha kuwa, Idara ya Ustawi wa Jamii kwa Wilaya ya Wete, mwaka 2011 ilipokea kesi 12, mwaka 2012 kesi tisa na kati ya Januari na Machi, 2013, matukio matatu yameripotiwa.
Kwa upande wa wilaya ya Newala, Katibu wa Mtandao wa asasi zisizokuwa za kiserikali Wilaya ya Newala mkoani Mtwara, Halima Nambunga, anasema asilimia 60 ya familia wilayani humo zinalelewa na bibi au mzazi mmoja kutokana na kutelekezwa au talaka za mara kwa mara.
Mkuu wa wilaya hiyo, Christopher Magala, anasema utamaduni wa kusafisha ghala au kuanua umechangia kuongezeka kwa tatizo. “Huu ni utamaduni ambao mwanaume wa Newala anapopata fedha hasa wakati wa msimu wa korosho, hutoa vitu vyote vya zamani ndani ya nyumba yake akiwamo mwanamke na kuingiza vitu vipya ikiwamo kuoa mwanamke mwingine,” alisema Magala.
Magala anafafanua kuwa utamaduni huo humsababishia mwanamke kutothaminiwa kwa kuwa utamaduni huo umekuwa ukiwadhalilisha wanawake na kuyumbisha watoto, kwani wakati huo mtoto atabaki na mama peke yake au kupelekwa kwa bibi yake na hatma yake watoto kukosa huduma muhimu kutoka kwa wazazi wao.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Newala, Samwel Maeda, anasema Sheria ya Matunzo kwa mtoto imepitwa na wakati kwani hadi sasa faini kwa mwanaume anayemtelekeza mtoto ni sh. 10,000 jambo ambalo wengi huipuuzia kwani wanafahamu kwamba watamudu kuilipa.
Kwa msingi huo, inashauriwa kuwa ipo haja kwa sheria hiyo ifanyiwe marekebisho ili iendane na wakati pamoja na uzito wa kosa lenyewe.
Watendaji wa vijiji vyote katika Kata ya Mtibwa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, wanaeleza kuwa wanaume wengi huzitelekeza familia zao wakati wa njaa na kuhamia vijiji vya mbali, huku wakiwaacha wanawake kuhangaika kuzilisha na kuzitunza familia peke yao.
Hata hivyo, wanaume hao hurejea na kuungana na familia zao wakati wa mavuno. Mbaya zaidi, wanasema baada ya kurejea kwa wanaume hao, huchukua jukumu la kuuza mazao yaliyolimwa na wanawake na watoto wao na wakishapata fedha, baadhi yao huenda kuoa wanawake wengine na kuziacha tena familia zao.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kidudwe, Marco Mwakatundu, anasema amekuwa akipokea malalamiko ya wanaume kuzikimbia familia zao hasa katika kipindi cha njaa ambacho mara nyingi ni kati ya Machi na Mei ya kila mwaka.
Ofisa Mtendaji wa Lukenge wilayani Mvomero, Ally Kingu, anasema kuna umuhimu wa jamii kuelimishwa juu ya haki na wajibu wao katika familia.
“Wanawake wanahitaji kuelimishwa juu ya umuhimu wa kujitambua na vile vile wanaume nao ili wajue haki na wajibu wao katika familia,” anasema.
Hata hivyo, Mratibu wa Elimu Kata ya Nachingwea (MEK), Benedict Barnabas Nyuchi, anasema tabia ya baadhi ya wanawake ndiyo chanzo cha wao kutelekezwa kutokana na kuwajibu waume zao kwa lugha za kijeuri na dharau.
Kwa mfano, Benedict Barnabas Nyuchi anasema mwanamke anayemjibu mumewe kuwa watoto wote siyo wake eti kwa kuwa hana uwezo wa kuzaa watoto kama hao, ni dhahiri atamuudhi mumewe na kusababisha ugomvi.
Katika mazingira kama haya, ni dhahiri mwanaume hupatwa na hasira na kuamua kuondoka kumuacha mke na watoto kama si kumpa kipigo kikali.

No comments:

Post a Comment