01 August 2013

SAKATA DAWA ZA KULEVYA:WACHUNGAJI KITANZINI

  • MAJINA YAO KUSAMBAZWA BALOZI ZOTE NJE
  • SERIKALI YATANGAZA MSIMAMO WAKE


Na Waandishi Wetu
MAWAZIRI, wabunge, maaskofu, mapadri, wachungaji wanaohusika uagizaji na uuzaji dawa za kulevya wametakiwa kutubu, kujisalimisha kwa Rais Jakaya Kikwete, ndani ya wiki hii vinginevyo majina yao kusambazwa katika balozi zote duniani.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kipentekoste, William Mwamalanga, kutokana na wanafunzi wawili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na St.Gasper cha Morogoro kusalimisha kilo tano za heroine katika kongamano la kidini lililofanyika TAG Mbeya.
Mbali na kujisalimisha vijana hao walitaja mawaziri wawili, Naibu waziri mmoja, wachungaji, baadhi ya wabunge watatu wa viti maalum na wabunge wastaafu wanaomiliki biashara kubwa ndani na nje ya nchi.
Mchungaji Mwamalanga alisema wamesikitishwa na viongozi hao wakuu wa nchi ambao ndio wanatakiwa kuonesha mfano kwa Watanzania kupiga vita dawa za kulevya, lakini wao ndio vinara wakuu wa kuwatumia vijana hao kununua na kuyauza  kinachoshangaza zaidi ni watumishi wa dini, maaskofu, wachungaji nao kuhusika na biashara hii kwa kutumia jina la Mungu kwa namna tofauti na sote tunaonekana tunafanya hivyo,"alisema.
Mchungaji Mwamalanga alisema wiki hii ni ya viongozi hao wa dini na serikali kutubu kwa ukamilifu mbele za Mungu na ikiwezekana waache kazi hizo, kwani hawaitakii mema nchi na Taifa lote kwa ujumla."Hii wiki ya kutubu kwa mawaziri na wabunge waliotajwa pamoja na kutubu wajisalimishe wenyewe kwa Rais Jakaya Kikwete wamweleze kwamba wao ni mabingwa wa kuuza dawa za kulevya.
"Kama hawatafanya hivyo wiki ijayo tutaanika majina yao yote katika balozi mbalimbali duniani kwamba hawa ndio vinara wa dawa za kulevya Tanzania, hivyo wakifika katika nchi hizo wasiruhusiwe kufanya chochote wakamatwe," alisema.
Mchungaji Mwamalanga alisema kuwa kusudi la kuanika majina yao ni ili dunia iwatambue na kusisitiza kwamba wasipofanya hivyo wiki ijayo watasambaza majina yao duniani kote.
Alisema kuwa viongozi hao wa dini wanatakiwa kujitambua na ndipo waweze kutubu ili waweze kupokea nguvu ya Mungu kwa kutubu mbele zake.
Mc h u n g a j i Mwama l a n g a a m e w a o m b a m a a s k o f u , wachungaji, mapadri, mashekhe kuungana pamoja kuwafichua wenzao wanaohusishwa na tuhuma hizo kwa kuwa wanajulikana.
Naye Mchungaji wa Kanisa la Moroviani Iringa Abeid Mbisa alisema aliwashutumu viongozi hao wa dini kwa kutumia jina la Yesu vibaya na kwamba watumishi wote wa dini wanahusishwa na kashfa hiyo wakati hawahusiki.
"Wanatumia jina la Yesu vibaya ninawashauri wapumzike kufanya kazi ya Mungu na badala yake wafanye kazi nyingine na ikiwezekana watubu na kumtumikia inavyopaswa,"alisema.
Alisema vijana wamekuwa wakiharibiwa na watu ambao hawakuwategemea na badala yake wanapaka matope makanisa na Taifa zima kwa ujumla.
Naye Mchungaji wa Kanisa la TAG, Calvary Tempo, Daud Mwalonde alisema kitendo cha viongozi hao wa dini, pamoja na viongozi wa serikali kuhusishwa katika sakata hilo la dawa za kulevya kunadhoofisha nguvu ya Taifa.
Alisema vijana wanalala barabarani, wanakuwa na sauti ambazo sio zao na nguvu ya Taifa imekwisha kutokana na wengi kupoteza nguvu ya kufanya kazi kutokana na kutumiwa vibaya. "Ombi langu kama mtu ameamua kuwa mtumishi afanye kazi ya Mungu asifanye Taifa kuelekea pasipotakiwa na kama mtu ni mchungaji na kisha anashiriki kazi hizi aachane na huduma hiyo kwa sababu haitakii mema Tanzania," alisema.
Wakati huo huo, Tume ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, imesema ina majina ya vigogo ambao wanahusika na uuzaji na usambazaji wa dawa hizo ambapo wanachunguza kwa kina na pindi upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani.Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana wakati wa kukabidhi msaada wa fedha wa kiasi cha sh.milioni 2.5 kwa taasisi zisizo za kiserikali za Tandika Youth Handcraft Group (TAYOHAG) Kwaya ya Nazareti, Kamishna wa tume hiyo, Christopher Shekiondo, alisema kazi ya kupambana na dawa za kulevya inafanyika vizuri na kwamba hadi sasa wana majina ya vigogo wanaojihusisha na dawa hizo, lakini wanaendelea na upelelezi.
Alisema baadhi ya vigogo hao wengine watafikishwa mahakamani wengine wamekimbia nchi na wengine bado hawajakamatwa na wanaendelea kuw atu miavijana kufuata dawa hizonjeya nc hi.
“Tuna majina ya vigogo ambao wanajihusisha na mtandao wa dawa za kulevya, lakini hatuwezi kuwataja kwa majina kwa sababu lazima kwanza tufanye upelelezi wetu wa kina ili tuwakamate na kama wamefikishwa mahakamani hatuwezi kuwataja hadi kesi iishe na wananchi wengi wanataka kujua majina hayo ya vigogo,” alisema.
Alisema watu wanaokamatwa na dawa hizo ni wale wanaotumwa na vigogo hao na ndiyo wanaokumbana na mkono wa sheria kwani wabebaji wote ndio wanaokamatwa mara nyingi.Hata hivyo imekuwa vigumu kunasa wahusika wakuu ambao ndio wanaowatuma wasafirishaji hao. Alisema si kila Mtanzania anayekamatwa nje ya nchi akiwa na dawa za kulevya hutokea Tanzania, bali kutokana na wahusika kuwa na mtandao mkubwa ndani na nje ya nchi, wanachokifanya hutuma pesa ambapo mtu anaweza kutokea nchi nyingine akaenda Brazil na kisha kuchukua dawa hizo na kuziingiza nchini China.
Alisema hata hao wanaoingiza dawa hizo nchini wanapita viwanja mbalimbali vya ndege vya kimataifa hadi kufikia hatua ya kukamatwa. Alisema mwaka 2010 kumekuwepo na ongezeko kubwa la ukamataji wa dawa hizo za kulevya nchini wakiwemo vigogo kutoka nje ya nchi. “Kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2012 kumekuwa na ongezeko kubwa la ukamataji wa dawa hizo ambapo kiasi cha dawa hizo aina ya heroin kilikamatwa kilo zaidi ya 760 huku cocaine zilizokamatwa zikiwa zaidi ya kilo 340 huku takwimu zikonesha kuwa mwaka huu kila wiki dawa hizo hukamatwa,” alisema Shekiondo.
Pamoja na juhudi hizo lakini kuna vyombo vingi vinavyohusika na udhibiti wa dawa hizo hivyo lazima kila sehemu inayohusika na kazi hiyo iangaliwe ili kudhibiti zaidi.Alisema Watanzania 110 wamekamatwa nchini Brazil ambapo walikwenda kuchukua dawa hizo na wengine 35 wamekamatwa nchini China.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Tanzania Labour Party (TLP), Augustino Mrema, ameitaka Serikali kuwakamata vigogo wote waliotajwa katika kashfa hiyo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mrema alisema Tanzania inaiga sera za watu wa Marekani, h i v y o i k umb u kwe k uwa Marekani ilimkamata Jenerali Manuel Noriega aliyekuwa Rais wa Panama kwa kuunga mkono matumizi ya dawa za kulevya nchini mwake."Hivyo ni jukumu la Serikali, kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kuruhusu sheria kuchukuwa mkondo wake kwa wahusika wote kwani ni aibu kwa Taifa,"alisema Mrema.
Akifafanua zaidi alisema kama Serikali haijachukua hatua za haraka ikumbuke kuwa kashfa hiyo ndio iliyosababisha kupinduliwa kwa Serikali ya nchi ya Panama na kuongeza hata mataifa mengine yatatuchukia kwa kuendelea kukaa kimya.Alisema hata kama taarifa hizo hazina ukweli wa asilimia 100, lakini zina ukweli wa asilimia 80 na kuongeza kuwa kama wanataka ushahidi wa asilimia 100 basi wasubiri mpaka atakaporudi Yesu au Mtume Muhammad ili awathibitishie.
Alisema hali imekuwa mbaya sana katika nchi yetu, watu walionekana wakisafirisha Twiga kupitia uwanja wetu wa ndege na sasa wameamua kusafirisha dawa za kulevya, kupitia nchini.Mrema amevitaka vyombo vya habari kutaja hadharani majina ya watu wote wanaojihusisha na mtandao huo ili kutoa fundisho kwa wahusika wengine.
"Imefika wakati lazima tuwe majasiri kwa kuwataja majina hadharani, potelea mbali tutawaomba samahani baadae maana sasa hali inatisha,"alisema Mrema.Alisema ikiwa mawaziri na wabunge wanatajwa kuhusika na dawa za kulevya, halafu wenyewe wanakataa wakidai wanasingiziwa ni lini watakubali ukweli kila siku wanasingiziwa wao tu. 


14 comments:

  1. inasikitisha sana kwamba watenda maovu kama hayo badala ya kutajwa ili tuwafahamu,tuwaepuke na kupelekwa mahakamani majina yao tena yatapelekwa kwa rais!!!!! kufanya nini ili hali rais anayo yake na hajachukua hatua yoyote. wewe mwamalanga kwa unalotaka kufanya hakuna utakalokuwa umelisaidia taifa hili

    ReplyDelete
  2. JE NI KWELI RAIS WETU ANAYO NIA YA DHAATI YA KUPAMBANA NA TATIZO HILI NA MENGINEYO MENGI?SINA IMANI NA RAIS HATA CHEMBE.NCHI IKO KWENYE MATATIZO MAKUBWA SANA.

    ReplyDelete
    Replies
    1. swala la kupambana na tatizo la madawa ya kulevya ni la wote rais ni sehemu ya wananchi isipokuwa huyu mchungaji ni moga wa kutaja -mbona anaonekana kusemasema sana kwanza ana uhakika au anafata anayoambiwa na hao wasomi.wasomi gani wa chuo kikuu wanakubali kutumiwa kiasi hicho.weka wazi majina ila ujuwe kujitetea maana utakuwa umechafua watu kwa zege kali kuwasafisha utaweza?

      Delete
    2. kama huyu mchungaji ana nia ya dhati na anaipenda nchi yake ni vyema awataje hao watu otherwise itaonekana anatafuta umaarufu kwa kutumia majina ya watu.

      Delete
  3. Huo utaratibu unaosemwa wa kujisalimisha kwa Rais mimi siuoni kuwa ni mzuri.Sijui kama kweli hao watu na hizi taarifa ni za kweli,na huo utamaduni wa waovu(wenye dhambi kwa mujibu wa mchungaji huyo)kuwaelekeza kwa Mkuu wa nchi.Wajibu wa mchungaji/padri ni kutubisha roho na kaisari kazi ni kuadhibu mwili.Kwa hiyo mch apeleke majina kwa kaisari asihusike mambo ya sheria.mwili utaadhibiwa na roho itaenda mbinguni kwa sababu imetubu.

    ReplyDelete
    Replies
    1. kweli kabisa. rais naye anaweza kuwa muhusika

      Delete
  4. Nasikitika sana kwani hao ambao tunadhani tumewapa nchi kwa kutuongoza hao hao ndio ambao wanatuua jamani. sasa tufanyeje. Mkuu wa nchi , sasa gurudumu linakuangukia wewew. tumia rungu jitoe muhanga kwani ndio kazi yako ya kuokoa na kutetea nchi hii

    ReplyDelete
  5. Ningekuwa mimi mwenye runge ningepa mchana peupe kwa ambao watuulia taifa letu

    ReplyDelete
  6. Hivi sisi watz tuna laana gani? hata viongozi wa dini wana woga wa kukemea wadhambi mpaka rais atoe ruhusa hii imekaaje?. Aibu kwao wanatupoteza muda......

    ReplyDelete
  7. NI VEMA WOTE WALIOTAJWA WAJIUZULU ILI UCHUNGUZI UFANYIKE KWA UHURU NA UWAZI

    ReplyDelete
  8. wahusika ni wale wenye madaraka, wakitajwa nchi itayumba hivyo jukumu ni letu wananchi

    ReplyDelete
  9. nchi hii siyo kama wengi mnavyodhani. Mfanyabiashara ya madawa ya kulevya siyo kama muuza cd feki. rais yeyote wa nchi duniani, ndiye amiri jeshi mkuu na wala hapaswi kubezwa kama wengi mnavyosema. matatizo ya Tanzania yalikuwepo toka enzi za ukoloni, hata hivyo usidhani hata aje rais yupi matatizo yako yataisha kwa kumchagua yeyote awe rais, kwanza fanya kazi na ujitume. hili ndilo litakalokuondolea matatizo. vijana wa tanzania tuache kulalamika hata mambo ambayo sisi hatuna uwezo nayo. Mchungaji yupo sahihi kwani ametoa mda wa hao kutubu na kama hawatafanya hivyo sheria itachukua mkondo wake. Kilo tano siyo mchezo.

    ReplyDelete
  10. hiyo ni kweli,ni serikali na taasisi ya Urais ilaumiwe maana hao ndo wanawalea ndugu zao na marafiki wao ambao wako kwenye system wengine ni matajiri tu wa kutupwa wana support chama tawala cha CCM,wengine wako serikalini ni wazito marafiki wa karibu waliomweka madarakani rais ambao anawajua na sio wasafi, wengi wao wamepewa ahsante nyingi ni vigumu tena kwa mkuu wa nchi kuwasaliti,pengine hizo hizo pesa chafu ziliyumika kwenye kampeni,watu hawa hawaguswi na chombo chochote cha usalama wa nchi hii.

    ReplyDelete
  11. Tumechoka kusikia neno "Vigogo" wakati majina yao kamili hayatajwi. Huu ni usanii tu, hakuna umakini katika jambo hili kwa sababu wasemao ndiyo wahusika.

    ReplyDelete